OR-TAMISEMI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imeielekeza Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha inafuatilia ukamilishwaji wa miundombinu, maabara na vifaa vyake, katika shule zote 26 maalum za Sayansi za wasichana zilizojengwa nchini.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Justin Nyamoga, ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya kamati kukagua mradi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Geita, mojawapo ya shule 26 za Kitaifa za Sayansi zilizojengwa nchini.
Amesema kuwa ukamilishwaji wa miundombinu hiyo ni muhimu kwa kuwa utawasaidia wanafunzi kusoma kwa vitendo.
“Tumetoa muda mfupi sana wa kuhakikisha maabara hizo zinakamilika na zinatumika. Tuliomba shule zote 26 zipelekewe maelekezo ya kuhakikisha maabara zinakamilika na zinatumika, na tuliomba wizara ichukue hatua za dharura kuhakikisha vitendanishi vinapelekwa na vinakuwa vya kutosha,” amesema Mhe. Nyamoga.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema wamepokea maelekezo ya kamati na kusisitiza kuwa lengo la ujenzi wa shule hizo ni kuwawezesha watoto wa kike kusoma masomo ya Sayansi katika mazingira salama, yatakayowaepusha na vishawishi vinavyoweza kusababisha kukatisha masomo yao.
Aidha, Mhe. Katimba ametoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini ambao wamepokea mradi wa shule hizo kuhakikisha miundombinu inakamilika kwa asilimia 100 ili wanafunzi waliokwisha ripoti shuleni wapate mazingira bora ya kusomea.