Na Mwandishi Wetu, Njombe
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kutafuta fedha za kuwalipa fidia wananchi waliopitiwa na Miradi ya kufua Umeme ya Ruhuji na Rumakali ili wananchi hao wapishe maeneo hayo na waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku wakati miradi hiyo ikisubiri kutekelezwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye ni Mbunge wa Same Mhe. David Mathayo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme katika Mkoa wa Njombe, tarehe 16 Machi 2025.
Amesema Serikali itafute fedha za kuwalipa fidia wananchi walioathiriwa na miradi hiyo ili wananchi hao wapishe na meneo hayo na waendelee na shughuli zao zingine wakati serikali ikiendelea kutafuta fedha za kutekeleza miradi hiyo.
“ Tayari tathmini imeshafanyika kwa wananchi watakaoathiriwa na mradi huyo na gharama za kuwalipa zimefahamika,na wananchi wanayo hiyo taarifa, ni vyema sasa serikali ikatafuta fedha za kuwalipa fidia wananchi hao ili wakaendelee na Maisha yao mengine wakati juhudi za kutekeleza mradi hiyo zikiendelea kufanyika”, alisisitiza Mathayo.
Utekelezaji wa Miradi ya Ruhuji na Rumakali utaiwezesha nchi kupata megawati 500 za umeme ambazo zitaimarisha hali ya upatikanai wa umeme nchini.
Kamati hiyo imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupelekea umeme kwa wananchi wake kama alivyoahidi katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kusema kuwa ni jambo la msingi sana kwa kuwa wananchi wamekuwa wakisubiri umeme huo kwa muda mrefu na kwa miaka mingi .
Alifafanua kuwa kuna maeneo mengine ni magumu kufikika kwa kuwa hakuna miundombinu ya Barabara na ambayo wananchi wake walikuwa hawajahi kupata umeme huduma ya umeme tangu enzi za uhuru lakini kwa sasa wamepata umeme kutokana na umakini wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwajali wananchi wake.
Pamoja na mambo mengine amewapongeza Wakala wa Nishati Vjijini (REA) na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa kupelekea umeme katika Vijiji na Vitongoji vya Mkoa huo ambapo katika maeneo mengine umeme huo umefikishwa kwa asilimia mia moja licha ya kuwa na miundombinu mibovu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga, akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko,amesema Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zilizochini yake wamepokea maelekezo ya kamati hiyo pamoja na shukrani kwa niaba ya serikali, katika kutekeleza miradi ya Umeme.
Ameweka wazi kuwa shukrani hizo zinakwenda moja kwa moja kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ndiye amekuwa kinara katika kuhakikisha kuwa miradi ya Umeme inatekelezwa na anafahamika duniani kote kwa namna ambavyo anasimamia Nishati kwa kadri ya uwezo wake ili wananchi wengi wafikiwe na umeme.
Kuhusu suala la fidia amesema kuwa Serikali imekuwa ikilipa fidia kwa wananchi wote wanaopisha miradi mbalimbali inayoanzishwa nchini, ikiwemo hiyo ya Ruhuji na Rumakali yenye thamani ya shilingi Bilioni 63.
Akitolea mfano baadhi ya miradi ambayo wananchi wake wamelipwa fidia ambayo ni ule ya Tanzania – Zambia (TAZA), na mradi wa kupelekea Umeme wa Gridi Katavi.
Serikali ya imepanga kuhakikisha wananchi wake wanaendelea kupata umeme wa uhakika na katika Mkoa wa Njombe zaidi ya asilimia 98 ya vijiji vyote vina umeme ambapo vimebaki Vijiji tisa tu ambavyo changamoto zake zinatatuliwa ili navyo vipate umeme.
Pia kuendelea kusambaza umeme katika maeneo ya pembezoni na kuimarisha nguvu ya umeme ili wananchi wapate umeme mwingi wa kutosha kukidhi mahitaji yao.
Azma ya serikali ni kuhakikisha kuwa ikifikapo 2030 asilimia 75 ya wananchi wote nchini wawe wamepata umeme na waweze kutumia nishati safi ya kupikia.
“Kwa sasa Serikali iko hatua za mwisho katika kukamilisha mradi wa Julius Nyerere utakaozalisha Megawati 2,115, hivyo hivi karibuni itaaza kutekeleza miradi ya Ruhuji na Rumkali, azma ya serikali ni kuhakikisha inaongeza vyanzo vya uzalishaji wa umeme hivyo serikali inatafuta fedha ili kuanza utekelezaji wa miradi hiyo”, alisema Kapinga.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini REA, Mhandisi Jones Olotu amesema kuwa mwambao wa Ziwa Nyasa unamaeneo korofi ambayo hayafikiki kirahisi katika utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini kwa kuwa hakuna miundombinu ya Barabara.
Hivyo umetafutwa utaratibu maalum wa kumpata mkandarasi mahsusi wa kutekeleza kazi hiyo ambapo sasa kazi kufanya upembuzi yakinifu inaendelea na baada kukamilika kazi ya kusambaza umeme katika maeneo hayo itaanza na itakamilika kabla ya kufika mwezi wa Sita mwaka huu 2025 ambapo vijiji hivyo vyote vitakuwa vimewashwa Umeme.
Kwa upade Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) Renata Ndege amesema miradi hiyo Ruhuji na Rumakali itagharimu zaidi ya shilingi trilioni 4 kutekeleza miradi hiyo.
Miradi hiyo ikitekelezwa itaongeza upatikanaji wa umeme nchini pia itaboresha maendeleo ya uchumi, Ajira kwa wananchi,miundombinu ya barabara, pamoja na huduma za kijamii.