Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na kampuni ya Oryx Gas Tanzania Ltd, tarehe 14 Machi, 2025 imezindua zoezi la kusambaza mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa wakazi wa wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma ambapo jumla ya mitungi ya gesi 3,255 itasambazwa wilayani humo kwa bei ya ruzuku ya shilingi 20,000.
Mkuu wa wilaya ya Buhigwe, Mhe. Kanali, Michael Ngayalina amezindua zoezi hilo katika Kitongoji cha Kamazi na kupongeza Serikali ya Awamu ya Sita kupitia REA pamoja na msambazaji, kampuni ya Oryx Gas kwa kuanza kugawa mitungi hiyo na kutoa wito kwa Wananchi kuchangamkia fursa hiyo ya nishati safi.
“Naipongeza REA kwa kutekeleza Mradi huu, nawapongeza Oryx Gas kwa kushirikiana na Serikali katika kusambaza nishati safi kwa Wananchi wa vijijini” amesema Mhe. Ngayalina.
Imeelezwa kuwa utekelezaji wa Mradi huo wa kusambaza mitungi ya gesi kwa mkoa wa Kigoma ulianza rasmi tarehe 3 Machi, 2025 katika wilaya ya Kasulu ambapo hadi jana zaidi ya mitungi 2,000 ilikuwa imeuzwa kwa Wananchi.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Nishati Safi mkoa wa Kigoma kutoka REA; Mhandisi, Ramadhan Mganga amesema, Serikali kupitia REA imetenga fedha (Shilingi milioni 390) kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa kusambaza mitungi ya gesi (LPG) ya kilo 6 kwa mkoa wote wa Kigoma katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji; ambapo mitungi 19,530 itauzwa kwa Wananchi kwa bei ya ruzuku ya shilingi 20,000.
“Mpango huu wa kusambaza mitungi ya gesi ni mzuri na kama mnavyofahamu; Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mama Samia Suluhu Hassan aliuzindua rasmi, tarehe 27 Februari, 2025 mkoani Tanga na kutoa mwelekeo wa kuhakikisha Wananchi wanahamasishwa kutumia nishati safi, ambapo lengo hadi ifikapo mwaka 2034 angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi.” Amesema, Mhandisi, Mganga
“Lengo letu ni kuwawezesha Wananchi wa vijijini ili wapate nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi. Nawaomba Wanancha wafike kwenye vituo vya kuuzia mitungi, wakiwa na Vitambulisho vya NIDA kwa ajili kununua mitungi hii pamoja na vifaa vyake kwa bei ya ruzuku ya shilingi (20,000/=) tofauti na ambavyo wangenunua kwa shilingi (56,000)”. Amesisitiza Mhandisi, Mganga.
Wilaya zitakazonufaika na usambazaji wa mitungi hiyo ya gesi kwa mkoa wa Kigoma ni pamoja Kasulu, Uvinza, Kakonko, Kibondo, Kigoma na Buhigwe