Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki Ulisubisiya, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita tarehe 5 Machi, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, Dodoma.
Frank Mvungi
Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili yaendelea kuimarisha ushirikiano na Taasisi mbalimbali za kimataifa katika kufanya kambi za upasuaji, mafunzo kwa wataalamu wake, tafiti na misaada ya vifaa tiba.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Machi 5, 2025 kuhusu mafanikio ya Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi. Dkt. Mpoki Ulisubsya amesema katika kipindi hicho taasisi iliingia mkataba wa ushirikiano na Chama cha Madaktari cha nchini China (CMA) na hospitali ya Tian Tan ya Beijing Peking China katika kuendeleza fani ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.
“Tumeendeleza ushirikiano na hospitali ya Ramaiah ya Bengaluru India katika kuendeleza fani ya upasuaji wa kurekebisha mishipa ya damu kichwani pasipo kufungua fuvu la kichwa (Interventional Neuroradiology)”, amesisitiza Dkt. Ulisubisya
Akifafanua Dkt. Ulisubisya amesema, kutokana na ushirikiano huu wameweza kuingia mikataba na makubaliano kati ya MOI na Smart Tech Solutions kutoka Egypt kwa ajili ya mafunzo na tiba, mkataba huu uliingiwa mwaka 2022.
Makubaliano mengine kwa mujibu wa Dkt. Ulisubisya ni kati ya MOI na Chuo Kikuu cha Cornell kutoka Marekani kwa ajili ya ushirikiano tangu mwaka 2023 na kati ya MOI na Chuo Kikuu cha Kairuki kwa ajili ya kufundisha, makubaliano haya yaliingiwa mwaka 2023.
Makubaliano kati ya MOI na AO Alliance Foundation kutoka Switzerland kwa ajili ya tafiti na msaada wa vifaa vya kufundishia matibabu ya mifupa na majeraha. Makubaliano yameingiwa kwaka 2024.
Eneo jingine ni makubaliano kati ya MOI na Taasisi ya Taifa ya Usafirishaji (National Institute of Transport) kwa ajili ya tafiti. Makubaliano haya yaliingiwa mwaka 2024.
Makubaliano kati ya MOI na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa ajili ya tafiti, mafunzo na tiba, makubaliano haya yameingiwa mwaka 2025.
Makubaliano mengine ni kati ya MOI na Hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tosamaganga kwa ajili ya mafunzo na tiba, makubaliano haya yameingiwa mwaka 2025.
Vile vile, Taasisi imeendelea kuwa hospitali ya kufundishia ya College of Surgeons of East, Central and Southern Africa (COSECSA) katika fani za ubobezi wa mifupa kwa watoto, upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu na utoaji wa dawa za usingizi na ganzi tiba.
Kuhusu mipango ya baadae ya MOI ni kuendelea kuboresha huduma kwa viwango vya kimataifa, ujenzi wa hospitali ya kisasa ya utengamao katika kiwanja cha MOI chenye ukubwa wa hekari 10 kilichopo Mbweni Mpiji jijini Dar es salaam.
Mpango mwingine ni kusogeza huduma katika jengo ambalo lilikua linatumika na Hospitali ya Tumaini Upanga ili sehemu ya wagonjwa wa nje waanze kupata huduma katika jengo hilo na kupunguza msongamano.
Aidha MOI inaendeleza jitihada za kusogeza huduma karibu na wananchi katika mikoa ambayo hajafikiwa ambayo ni Tanga, Ruvuma, Kigoma,Geita, Njombe, Manyara, Mara na Kagera.