Featured Kitaifa

DC SHEKIMWERI APONGEZA JIJI LA DODOMA KUPANDISHA UFAULU

Written by mzalendoeditor

Na. Aisha Ibrahim, DODOMA

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, amewapongeza wadau na waratibu wa elimu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi ngazi ya msingi na sekondari unazidi kupanda kila siku katika Jiji la Dodoma.

Alitoa pongezi hizo katika kikao cha wadau wa elimu na kuutambulisha mfuko wa lishe shuleni wa mwaka 2025, kilichofanyika ukumbi wa Vijana uliopo Kata ya Kiwanja cha Ndege, jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho alisema kuwa, lengo la Rais wa awamu ya sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuanzisha mpango wa lishe bora shuleni ni kukuza ufaulu wa wanafunzi na kuenzi kauli za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, isemayo “Elimu tunayohitaji siyo tu ya kujua kusoma na kuandika bali ni elimu ya kujenga jamii yetu ya kufanya tuwe na uwezo wa kufanya kazi na kuleta maendeleo kwa wengine”.

Aliongeza kuwa, chini ya utawala wa Rais wa awamu ya sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali imejitahidi kuboresha na kutekeleza kwa vitendo mtaala mpya wa sera ya elimu ambapo matarajio ni kutoka kwenye elimu ya kukariri na kuvuka kwenda kwenye elimu ya kuelewa na kujua mambo kwa uhalisia wake. “Tunaona serikali chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeboresha mtaala mpya wa sera ya elimu, uliozinduliwa hapa jijini Dodoma, lengo ni kutoka zama za kusoma kwa kukariri na kwenda kwenye elimu ya kuelewa” alisema Alhaj Shekimweri.

Katika hatua nyingine, alifafanua kuwa “serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuongeza ajira kwa watumishi na kuboresha miundombinu kwa shule za msingi na sekondari kama vile madarasa mapya, nyumbani za walimu, matundu ya vyoo vya wanafunzi na walimu, maabara za kisasa kwa shule za sekondari. Hivyo, kwa muktadha huo hatutegemei ufaulu unaopungua dalaja la kwanza” alisema.

Aidha, aliwaasa wazazi na walimu kusimama katika ubora wao kuhakikisha Jiji la Dodoma linatokomeza ufaulu wa daraja la nne na  sifuri kwasababu serikali imeboresha miundombinu na maslahi ya wasimamizi wa elimu.” Kila mmoja hapa kwa nafasi yake  akisimama kidete, basi Jiji la Dodoma hakutakuwa na daraja la nne wala sifuri kwasababu serikali imejitahidi sana kuwaletea miundombinu rafiki na maslahi ya kila mtu” alisema Alhaj Shekimweri.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Alkan Mwanga, alieleza kuwa lengo la kuboresha mtaala wa elimu nchini Tanzania ni kuendana na mabadiriko mbalimbali ya nchi na utandawazi kiujumla. “Lengo la kuboresha mtaala huu ni kuweza kuendana na mahitaji ya jamii, mabadiliko ya Sayansi na teknolojia na maendeleo ya mabadiriko ya kisiasa” alisema Mwanga.

Sambamba na hayo alifafanua muundo wa mtaala mpya wa elimu na kusema kuwa muundo huo hujumuisha kuondolewa kwa mtihani wa darasa la Saba, upimaji wa mtihani wa kitaifa kufanyika Darasa la Sita, mwanafunzi atatakiwa kumaliza kidato cha Nne kabla ya kuweza kujiajiri au kuajiriwa. Pia kuwepo kwa mikondo miwili katika ngazi ya sekondari yaani mkondo wa jumla na mkondo wa amali (ufundi). Wanafunzi wataweza kuchagua mkondo unaowafaa kulingana na uwezo wao na malengo yao na wahitimu kutoka mkondo wa amali watapata vyeti viwili: cheti cha ufundi pamoja na cheti cha masomo ya jumla ambayo ni muhimu kwa ajili yao kujiajiri au kupata ajira serikalini, alifafanua.

Maboresho ya mtaala mpya wa elimu nchini Tanzania yanatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu, na yamepangwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2025 ambapo lengo kubwa ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata maarifa yanayohitajika katika soko la ajira.

About the author

mzalendoeditor