Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, akizungumza na waandishi wa Habari leo Februari 21,2025 katika Chuo Cha VETA Mkoani Singida kuelekea maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanziahwa Kwake mwaka 1995
………
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetangaza rasmi maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1995.
Akizungumza na wanahabari leo, tarehe 21 Februari 2025, katika Chuo cha VETA Singida, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema maadhimisho hayo yataangazia mafanikio, changamoto, na mustakabali wa elimu ya ufundi stadi nchini.
CPA Kasore amesema kuwa katika kipindi hiki vyuo vya VETA vilivyoenea kwenye mikoa na wilaya nchini kote vitatoa huduma ya ufundi bure ya ukarabati wa miundombinu ya Serikali kama majengo ya hospitali, zahanati, shule, ofisi za umma pamoja na kwa watu wasiojiweza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho na kuonesha mchango wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwenye jami.
_“Wanafunzi, walimu na wahitimu watatoa huduma za kiufundi kama kupaka rangi majengo yaliyochakaa, kurekebisha mifumo ya umeme, mifumo ya mabomba ya maji, milango na samani,”_ amesema.
Katika hotuba yake, CPA Kasore amesema kuwa maadhimisho haya yanajikita katika kutambua mchango wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika maendeleo ya taifa, kufanya tathmini ya safari ya VETA kwa miaka 30, na kujadili mwelekeo wa sekta hiyo kwa miaka ijayo. Aidha, amesisitiza kuwa maadhimisho haya yataimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo ya elimu ya ufundi.
Amesema kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika kwa siku nne, kuanzia Machi 18 hadi 21, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ambapo kutakuwa na maonesho ya kazi na ubunifu wa wanafunzi, mashindano ya ujuzi, kongamano la wadau, na utoaji wa tuzo kwa taasisi na watu binafsi waliochangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya ufundi stadi nchini.
CPA Kasore amesema: _“Miaka 30 ya VETA ni ushuhuda wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha vijana wa Tanzania wanapata ujuzi bora wa ufundi stadi unaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa. Katika miaka hii, tumeweza kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa.”_
Amesema, kwa miaka 30, VETA imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mifumo ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa kujenga vyuo vipya, kupanua fursa za mafunzo kwa makundi maalum, na kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Amefafanua kuwa idadi ya vyuo vinavyomilikiwa na VETA imeongezeka kutoka 14 mwaka 1995 hadi 80 mwaka 2025, huku vyuo vingine 65 vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi. Aidha, sekta za mafunzo zimeongezeka kutoka 10 mwaka 1995 hadi 13 mwaka 2025, zikihusisha fani 89 zinazohitajika katika maendeleo ya viwanda na uchumi wa kisasa.