Jopo la Wanasheria wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria wakiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Haki za Binadamu Bi. Beatrice Mpembo Februari 19, 2025 Jijini Mwanza wamefanikiwa kutatua changamoto ya ardhi iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Kata ya Nyamagana.
Hayo ya yamejili kufuatia utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) Jijini hapo ambapo majirani hao Johanes Johnbosco na Bw. Yassin Suleiman walitofautiana kwenye matumizi ya ardhi.
Imeelezwa kwamba Bw. Johanes aliingia makubaliano ya kuchimba na kujenga shimo la maji taka katika eneo la Jirani yake huyo kupitia kwa mmiliki wa awali wa eneo hilo baada ya Bw. Johanes kukumbana na changamoto ya mwamba katika eneo lake.
Hata hivyo shimo hilo limekuwa likitumiwa kwa Pamoja na mmiliki wa awali hadi mmiliki wa sasa kabla ya kupishana na kumtaka Bw. Johanes kuacha kutumia shimo hilo
Baada ya wanasheria hao kufika eneo la tukio wamefikia maridhiano kuwa kwa sasa waendelee kutumia Pamoja huku Bw. Yassin akitoa kipande cha Ardhi yake kumpatia Johanes ili ndani ya miaka mitatu ajenge shimo lake katika kipande hicho.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid) inaendelea katika Halmashauri zote Nane za Jiji la Mwanza ambapo wataalamu wa Sheria wanaendelea kutoa elimu na kutatua migogoro mbalimbali.