Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya wazazi CCM wilaya Shinyanga Mjini wakitembelea Daraja la Chibe – Old Shinyanga
Wajumbe wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini wameeleza kuridhishwa na ujenzi wa miradi ya madaraja katika kata za Chibe na Ibinzamata, wakisema kuwa miradi hiyo ni kielelezo tosha cha namna fedha zinazotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinavyosaidia kuboresha miundombinu ya barabara.
Wakiwa katika kata za Chibe na Ibinzamata leo Februari 20,2020 ikiwa ni sehemu ya ziara yao ya kutembelea kata zote za Jimbo la Shinyanga Mjini, Wajumbe hao, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, wamesema uboreshaji wa miundombinu ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
“Tumeliona daraja linalounganisha Chibe na Old Shinyanga, ni zuri, limejengwa na mhandisi mahiri, linaunganisha kata ya Chibe na Old Shinyanga na maeneo mengine kama Mwawaza hadi. Daraja hili ni zuri na tunaenda kuifanyia kazi ombi la diwani kuwekewa taa kwenye daraja hili ili kuimarisha usalama kwa wanaopita nyakati za usiku,” amesema Mrindoko.
“Tumejionea pia ujenzi unaoendelea wa daraja la Ibinzamata Makaburini. Daraja hili linajengwa vizuri. Tunawapongeza viongozi wote mliofanikisha kujengwa kwa daraja hili ili kurahisisha usafiri, lakini pindi tatizo la msiba linapotokea, wananchi waweze kupita kwa urahisi kwenda kuwahifadhi ndugu zetu waliotangulia mbele za haki. Ujenzi unaendelea vizuri na lipo katika hatua za ukamilishaji,” ameeleza Mrindoko.
Mrindoko ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya barabara, elimu, maji, afya n.k.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe, amesema ujenzi wa daraja kubwa la Chibe ni sehemu ya kazi nzuri zinazofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha miundombinu ya barabara inakuwa mizuri ili kuwezesha kukua kwa uchumi.
“Daraja la Chibe ni kubwa na zuri. Haya ni mambo mazuri yanayofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan. Mama Samia ametekeleza Ilani ya CCM kwa zaidi ya asilimia 100. Ameonesha maendeleo ya kiuchumi kwa vitendo, nasi hatuna zawadi ya kumpa zaidi ya kumpatia kura za kutosha kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2025 kwa sababu tayari Chama kimempitisha kuwa mgombea Urais kupitia CCM pamoja na mgombea mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi ili waweze kutuletea maendeleo zaidi,” amesema Jumbe.
Jumbe ametumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania kuendelea kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwakaribisha waliopo katika vyama vya upinzani na wasio na chama kujiunga CCM kwani ni chama imara chenye ni ya dhatiya kuwaletea maendeleo wananchi.
“Mwaka 2020 Shinyanga tulikuwa wa pili katika kukipigia kura kwa Kishindo Chama Cha Mapinduzi, mwaka huu 2025 tunataka tushike nafasi ya kwanza. Nafasi ya Urais tayari tuna mgombea Mama yetu Mhe. Samia Suluhu Hassan, nafasi za Udiwani na Ubunge wagombea watapatikana kwa mujibu wa taratibu za Chama,” ameongeza Jumbe.
Diwani wa kata ya Chibe, Mhe. John Kisandu, amesema ujenzi wa daraja la Chibe – Old Shinyanga lenye urefu wa mita 45 lililopo katika Mto Mkubwa, linalojumuisha barabara, kalvati na daraja likigharimu jumla ya shilingi Milioni 475, umekamilika na lipo katika matazamio huku akiomba taa ziwekwe katika eneo hilo ili kuimarisha usalama wapitaji kwani linatumiwa na watu kutoka maeneo mengi, ikiwemo kutoka Mkoani Tabora.
Diwani wa kata ya Chibe, Mhe. John Kisandu, akielezea kuhusu ujenzi wa daraja la Chibe – Old Shinyanga
“Daraja hili limerahisisha mawasiliano kati ya kata ya Chibe na Old Shinyanga, kwa sababu hapa palikuwa hapapitiki wakati wa masika kutokana na kuwepo kwa mto mkubwa. Usalama sasa upo na mapato ya Halmashauri yameongezeka kutokana na kwamba sasa wafanyabiashara wengi wanaokwenda katika Mnada wa Old Shinyanga na Tinde wanapita katika daraja hili,” ameeleza Kisandu.
Naye Diwani wa kata ya Ibinzamata, Mhe. Ezekiel Sabo, amesema ujenzi wa Daraja la Ibinzamata Makaburini linasaidia kurahisisha kufika katika eneo la Makaburini na maeneo ya jirani kwani eneo hilo lilikuwa halipitiki wakati wa masika baada ya daraja la awali kuvunjika.
Wajumbe wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini inaendelea na ziara ya kutembelea kata za Jimbo la Shinyanga Mjini, lengo kuu ni kuzungumza na wanachama na viongozi wa CCM, kufanya tathmini ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, kuangalia hali ya uhai wa chama, na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo hayo.