Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali inaitazama Tume kama taasisi nyeti na ya kimkakati katika utatuzi wa migogoro ya kikazi nchini ikiwa na lengo la kuchochea ukuaji wa kiuchumi na kuhakikisha mahala pa kazi panakuwa na amani ili kuwafanya wafanyakazi na waajiri watumie muda mwingi kufanya uzalishaji wenye tija.
Ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Tathmini ya Utendaji Kazi na mafunzo kwa watumishi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Tanzania bara, kilichofanyika Leo tarehe 19 Februari, 2025 Mkoani Morogoro.
Aidha, ameitaka Tume kushughulikia migogoro kwa haraka, ufanisi na weledi ili kuweza kutimiza matarajio ya wadaawa na wadau ambao wengi wao ni wawekezaji, hivyo kusaidia kukuza Uchumi wa nchi.
“Serikali iliongeza bajeti ya Tume kiasi cha zaidi ya Shilingi Milioni mia tisa (900,000,000+) bila shaka mmeona ongezeko hilo limeleta mabadiliko siyo tu kwenye maslahi ya wafanyakazi lakini pia kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake ya msingi” amesema Mhe. Ridhiwani Kikwete.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, amewakumbusha wasuluhishi na waamuzi kutilia mkazo suala la matumizi ya mfumo wa kieletroniki na hususani kuangalia namna bora ya kupokea vielelezo ili kuwasilisha jalada kamilifu pindi litakapoitishwa mahakamani.
Naye, Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mhe. Usekelege Mpulla kwa niaba ya menejimenti ya Tume, amemshukuru Mhe. Ridhiwani Kikwete Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa namna anavyosimamia na kutoa miongozo kwa maslahi ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.