Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe, ameweka wazi imani yake kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza leo katika ziara ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Old Shinyanga na Mwamalili, Mhandisi Jumbe amesema kwamba Rais Samia ameonesha uongozi thabiti na mafanikio katika sekta muhimu, akiboresha miundombinu, elimu, afya, na kutoa mikopo kwa makundi maalum, ikiwa ni ishara ya maendeleo endelevu kwa wananchi.
“Rais Samia ni mtu anayetaka maendeleo, amekuwa akiboresha miundombinu, uboreshaji huu wa miundombinu ya barabara unasaidia kwa kiwango kikubwa sana kuhakikisha uchumi wetu unakua kwa kasi kubwa,” amesema Mhandisi Jumbe.
Aidha, Mhandisi Jumbe amezungumzia hatua muhimu zilizochukuliwa na Rais Samia katika sekta ya afya, ambapo amewezesha upatikanaji wa vifaa tiba, majengo ya hospitali, vituo vya afya na zahanati.
Hali kadhalika, amesema Rais Samia amekuwa na juhudi kubwa katika kuboresha elimu, akiongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu na kuajiri walimu kwa wingi.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Jumbe ameeleza umuhimu wa mshikamano ndani ya CCM, akisema kuwa umoja wa wanachama utawezesha chama kuendelea kushika dola na kuboresha maisha ya wananchi.
Ametoa wito kwa wanachama na viongozi wa chama kuendelea kuwa na umoja na mshikamano ili kuhakikisha ushindi wa CCM, akisisitiza kuwa mchakato wa utekelezaji wa Ilani ya CCM chini ya Rais Samia Suluhu Hassan umeonesha mafanikio makubwa.
“Tushirikiane kwa nguvu, tuendelee kujenga chama, tuunge mkono Rais wetu na viongozi wa chama, na tupate ushindi mkubwa,” ameongeza.
Mhandisi Jumbe pia amesisitiza kuwa utendaji wa Rais Samia katika utekelezaji wa Ilani ya CCM umekuwa wa kiwango cha juu, ndiyo maana wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM walimpendekeza kwa kauli moja kuwa awe mgombea pekee wa Urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu wa 2025.
“Mheshimiwa Rais Samia anatekeleza majukumu yake kwa weledi mkubwa na amefanya kazi pasipo kuchoka ndiyo maana mkutano mkuu wa CCM wajumbe walipitisha azimio la mkutano mkuu kumpitisha kuwa ndiye Mgombea pekee wa Urais kupitia CCM.
Hakupitishwa kwa sababu yeye ni mwanamke au kwa sababu tu yeye ni mkuu wa nchi ana vyombo vya ulinzi na usalama lakini utekelezaji wa Ilani, watu waliridhika nao na ndiyo maana wajumbe wa mkutano mkuu, kupitia maoni ya wanachama mbalimbali walipendekeza Dkt. Samia Suluhu Hassan awe mgombea Urais lakini pia Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza ambaye amefanya kazi kubwa katika chama hata katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Mhe. Nchimbi ni mchapakazi, muungwana, mwenye heshima, mstahimilivu. Kwa hiyo ukiangalia huo muungano (combination) ya Dkt. Samia na Dkt. Nchimbi hakuna mashaka kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka huu, tunaenda kushinda kwa kishindo,” ameongeza Jumbe.
Amempongeza Rais Samia kwa jitihada zake zisizo na kipingamizi na kusema kuwa ushindi wa CCM umehakikishwa.
Kwa upande mwingine, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kujenga chama na kuhamasisha wananchi kujiunga na CCM, huku akisema kuwa chama kinahitaji michango ya wanachama wake ili kuendelea kukua na kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.
Mhandisi Jumbe pia amekumbusha jamii umuhimu wa malezi bora kwa watoto, akisema kuwa ni muhimu kuwa karibu na watoto, kuwaongoza, na kuwakinga dhidi ya vitendo vya unyanyasaji ili kujenga taifa lenye matumaini.
Mhandisi Jumbe amewahakikishia wanachama wa CCM na Watanzania kwa ujumla kuwa chama hicho kipo tayari kuendelea kutekeleza ilani yake kwa ufanisi mkubwa, na kwamba uchaguzi mkuu wa 2025 utashuhudia ushindi mkubwa kwa CCM.
Akizungumza kwenye ziara hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia na kutambua juhudi zake za kuboresha ustawi wa taifa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko
“Msikubali kupotoshwa, nchi hii imejengeka. Hawa wanaokuja kubeza leo wametoka wapi? Tumshike mkono Mama Samia, tumpe mitano tena, amefanya mambo mazito, tusimame pamoja naye. Mama huyu amefanya mambo mazuri sana. Naomba msimame imara, hakuna mtu wa kuwayumbisha na kuwatoa kwenye mstari mkamuacha Samia,” amesema Mrindoko.
Amesema pia ni muhimu kupuuza watu wanaobeza mafanikio ya Rais Samia, akitaja baadhi yao kama “washamba” wanaopuuza maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika sekta muhimu kama vile miundombinu, elimu,maji, umeme na afya.
“Tuwapuuze hawa washamba wanaopuuza kazi nzuri zinazofanywa na Mama Samia katika sekta mbalimbali. Watanzania tuendelee kuwa macho na kushirikiana kwa pamoja ili kutimiza malengo ya maendeleo,” amesema Mrindoko.
Pia, amezungumzia umuhimu wa kulinda watoto dhidi ya vitendo vya ubakaji na ulawiti, akisema: “Hawa wanaolawitiana na kusagana ni dhambi kubwa kwa Mungu. Tukatae hii tabia ya watoto wetu kuchezewa chezewa, tukabiliane na hawa wanaochezea watoto wetu, wanaolawiti na kubaka watoto wetu.”
Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Dorice Kibabi, amesisitiza umuhimu wa mshikamano miongoni mwa wanachama wa CCM, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Dorice Kibabi
Kibabi pia amehamasisha wananchi kujiunga na chama na kulipa ada ya uanachama CCM, akisema kuwa uhai wa chama unatokana na michango ya wanachama ikiwemo kulipia kadi ya uanachama.
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe akizungumza wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati ya utekelezaji wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Mwamalili na Old Shinyanga.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, akizungumza katika ziara yake na wajumbe wa kamati ya utekelezaji wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Mwamalili na Old Shinyanga.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Dorice Kibabi, akizungumza wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati ya utekelezaji wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Mwamalili na Old Shinyanga.
soma pia
WAZAZI CCM SHINYANGA MJINI WAMPONGEZA RAIS SAMIA ….’MSIKUBALI KUPOTOSHWA’