Featured Kitaifa

SERIKALI: UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI ZANZIBAR YAFIKIA ASILIMIA 98

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu maswali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Ameir Abdallah Ameir, aliyetaka kujua miradi ya umwagiliaji inayofadhiliwa na Mashirika ya Kimataifa na la Mbunge wa Buyungu, Mhe. Aloyce Kamamba aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kufungua Kituo cha Forodha katika Kijiji cha Muhange, Nyabibuye na Malenga ili kuongeza kipato kupitia forodha mipakani.

(Picha na Kitrngo cha Mawasiliano Serikalini WF -Dodoma)

Na. Josephine Majura WF-Dodoma

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imenufaika na ufadhili wa mashirika ya kimataifa katika miradi ya umwagiliaji inayolenga kuongeza uzalishaji wa kilimo na kuboresha maisha ya wakulima wa Zanzibar.

Ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Ameir Abdallah Ameir, aliyetaka kujua miradi ya umwagiliaji inayofadhiliwa na Mashirika ya Kimataifa Zanzibar.

Mhe. Chande alisema miongoni mwa miradi inayotekelezwa Zanzibar kupitia fedha za Mashirikia ya Kimataifa ni Mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Umwagiliaji Zanzibar, ambao unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Exim ya Korea (EDCF), ambapo umefadhiliwa kupitia Mkopo wa awali wa USD 50m na Mkataba wa nyongeza wa USD 18.1m

Aliongeza kuwa, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 98, na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 8 Juni 2025. 

Katika hatua nyingine, Mhe. Chande alisema katika kuhakikisha kuwa Serikali inatatua changamoto ya kukosekana kwa huduma za kiforodha katika vijijiji vya Muhange, Nyabibuye na Malenga, Serikali imepeleka Maafisa wa Forodha wawili (2) eneo Muhange kwa ajili ya kutoa huduma za kiforodha.

Alisema kuwa maafisa wanaohudumia Kituo cha Nyaroga wataanza kuhudumia Nyabibuye kwa awamu kabla ya kufungua Ofisi ya kudumu na eneo la Malenga litahudumiwa na maafisa kutoka Muhange.

Mhe. Chande alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Buyungu, Mhe. Aloyce Kamamba aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kufungua Kituo cha Forodha katika Kijiji cha Muhange, Nyabibuye na Malenga ili kuongeza kipato kupitia forodha mipakani.

About the author

mzalendoeditor