OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewataka Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wabunge wanapangiwa ratiba ya kuzindua miradi yote ambayo haijazinduliwa katika majimbo yao.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati wa kuchangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024, Mhe. Mchengerwa amesema wabunge wamekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha upatikanaji wa miradi hiyo.
“Ipo miradi inaendelea katika majimbo yetu, na kwa muda tuliobaki nao ni dhahiri kwamba viongozi wakuu wa nchi na mawaziri hawawezi kufika kila jimbo kukagua na kuzindua miradi hiyo. Kwa kuwa tuna miradi mingi, nawaelekeza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuwapangia wabunge miradi yote ambayo haijazinduliwa ili waende wakaizindue mara moja katika majimbo yote 215,” amesema Mhe. Mchengerwa.
Pia amesisitiza kuwa Wabunge wamekuwa na mchango mkubwa katika upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo ndilo chombo kinachotunga sheria na kupitisha bajeti ya nchi.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amepongeza kazi kubwa inayofanywa na watendaji wa sekretarieti za mikoa, Halmashauri na Tarafa katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye sekta za elimu, afya, miundombinu na maji kote nchini.