Mkurugenzi wa Mifumo,Tathmini na Mawasiliano wa TASAF Bw.Japhet Boaz,akizungumza wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya bodi ya mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu yaliyoambatana na uzinduzi wa Maonesho na huduma kwa wateja yanayofanyika jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
JUMLA ya wanafunzi 11,524 kutoka Kaya maskini zilizotambuliwa na Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu kwa asilimia 100 kwa ajiri ya kuendelea na masomo katika vyuo mbalimbali hapa nchini.
Hayo yameibainishwa leo Februari 10,2025 na Mkurugenzi wa Mifumo,Tathmini na Mawasiliano wa TASAF Japhet Boaz,wakati akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya bodi ya mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu yaliyoambatana na uzinduzi wa Maonesho na huduma kwa wateja yanayofanyika jijini Dodoma.
Bw.Boaz amesema ,TASAF na HESLB ziliingia makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na kuweza kuunganisha kazidata zake ili kuwezesha waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kaya za Walengwa kutambulika kirahisi na kuwa wanufaika wa Mikopo hiyo ya elimu ya juu kwa asilimia 100.
Amesema kuwa wameishkuru serikali kupitia bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa kutambua na kuendeleza rasilimali watu kutoka Kaya maskini katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Idadi hiyo ya wanafunzi waliopata mkopo huo ni tokea mwaka 2019/2020 hadi 2024/2025, kitendo ambacho kimepelekea watoto hao kutimiza ndoto zao za kujiendeleza kielimu pamoja na kuwa wametoka katika kaya maskini.”amesema Bw.Boaz
Aidha amesema kwa kipindi cha miaka 10 TASAF imeweza kuzitambua, kuziandikisha na kuzipatia ruzuku yenye masharti, zaidi ya kaya maskini milioni 1.2 zenye zaidi ya wanakaya milioni 5.2 nchini kote katika vijiji, mitaa yote ambapi alusema miongoni mwa wanakaya tajwa kuna watoto 724,867 wanaosoma shule za msingi, wakati 341,827 wamasoma sekondari (O-level) na 26,308 (A-level).
“TASAF unaendeleza juhudi za Serikali katika kupunguza umaskini kwa kaya zenye upungufu wa mahitaji ya msingi ili kuziwezesha kaya hizo maskini kuongeza kipato, fursa za kiuchumi na uwezo wa kugharimia mahitaji muhimu na zaidi kujenga rasilimali watu.”amesema
Hata hivyo amesema Mfuko huu unasaidia kujenga miundombinu kwenye Jamii zenye upungufu wa huduma hizo katika sekta za Elimu, Afya, Barabara vijijini na Miundombinu mingine ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wanachi na hasa kaya maskini.
Pia amesema kuwa kaya zenye watoto walio katika umri wa kwenda shule wanalazimika kuhakikisha watoto wao wanahudhuria masomo kwa asilimia zaidi ya 80% ya siku za masomo ili wapate ruzuku hiyo na kuongeza kuwa jambo hilo limepelekea watoto wengi kutoka kaya za Walengwa kuwa na maendeleo mazuri ya kitaaluma na kuweza kufaulu masomo yao vyema kwa alama zinazowawezesha kuingia katika vyuo vya elimu ya juu.
Afua zingine zinazotekelezwa na TASAF ni pamoja na kujenga Miundombinu kwenye sekta ya Maji, Afya, Elimu na Mazingira; pamoja na kuwawezesha wanufaika wa mpango kuunda vikundi vya kuweka akiba na kupeshana pamoja na kutoa ruzuku ya uzalishaji kwa walengwa ambao wameanzisha bashara au shughuli za kuongeza kipato.
Amesema kwa ujumla wa afua hizi zimeweza kusaidia zaidi ya kaya 400,000 kuhitimu katika Mpango na kaya hizi zinaendelea na shughuli zake na si maskini tena. Haya ni mafanikio makubwa na ya kujivunia ambao yanaashiria matokeo chanya ya Utekelezaji wa Mpango.