Featured Kitaifa

USHIRIKI WA WANAWAKE NA WASICHANA KATIKA FANI YA SAYANSI NI MDOGO – MHE. KIPANGA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga amesema takwimu za elimu na ajira duniani zinaonesha kuwa ushiriki wa wanawake na wasichana katika elimu na ajira katika fani za sayansi ni mdogo ikilinganishwa na ushiriki wa wanaume hali ambayo inapunguza juhudi za kufikia usawa wa kijinsia katika elimu na ajira.

Naibu Waziri Kipanga ameyasema hayo leo Februari 7,2025 hapa Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya kitaifa ya siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi ambayo huadhimishwa Fruari, 11 kila mwaka.

“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya umma na binafsi, imeandaa maadhimisho haya ambapo kwa mwaka huu 2025, hafla ya Kitaifa ya kuadhimisha siku hiyo itafanyika siku ya Jumanne tarehe 11, Februari, katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), Jijini Dodoma, na Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Prof. Adolf Mkenda,”amesema.

Amesema Tanzania inatambua kuwa usawa wa kijinsia ni muhimu kwa kufikia malengo ya maendeleo yaliyokubaliwa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, kutokana na maazimio hayo ya Umoja wa mataifa, Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi kuanzia mwaka 2021.

“Lengo la kuadhimisha siku hii, ni kutambua na kusherehekea mchango wa wanawake na wasichana katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), maadhimisho haya ni fursa ya kuhamasisha wanawake na wasichana zaidi kujiunga katika nyanja hizi ili kubadili mustakabali wao na jamii zetu kwa ujumla. Masuala ya wanawake na wasichana ni mtambuka na hivyo yanahitaji ushiriki na mchango wa wadau wote bila kujali wako katika sekta ya umma au binafsi,”amesema.

Sanjari na hayo Kipanga ameongeza kuwa kupitia maadhimisho ya mwaka huu wanaendelea kuhimiza juhudi mbalimbali zinazokusudiwa katika kuimarisha uelewa wa watanzania kuhusu umuhimu wa kushirikisha wanawake na wasichana katika uongozi na maamuzi juu ya masuala ya sayansi.

Pia, amesema wanahitaji kuhamasisha kizazi kilichopo na kijacho cha wasichana kupenda na kujiunga na masomo ya sayansi kwa kuondoa dhana potofu na kutoa fursa sawa katika elimu na maendeleo ya kitaaluma.

“Tunahitaji mifumo madhubuti ya ushauri na usaidizi katika kukuza vipaji vya wanawake na wasichana wanaotaka kufikia ndoto zao za kuwa wanasayansi mahiri, hivyo ningependa kutoa wito kwa jamii nzima kushirikiana katika kuhamasisha ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi na teknolojia,”ameongeza.

Amesema Wazazi, walimu, viongozi wa dini na kijamii, na wadau wote tuna wajibu wa kuhakikisha wasichana wanapata elimu bora na fursa sawa za kujihusisha na nyanja hizi, hivyo kwa pamoja wanaweza kubadili mustakabali wa taifa kwa kuhakikisha wanawake na wasichana wanachangia kikamilifu katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Baraza Kuu la Umoja wa mataifa mwaka 2015, lilipitisha programu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi kwa kutangaza tarehe 11 Februari kuwa Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika sayansi. 

About the author

mzalendo