Featured Kitaifa

MWITIKIO WA WANANCHI WIKI YA SHERIA WAMKOSHA KATIBU MKUU KATIBA NA SHERIA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu,  Dodoma. 

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi amevutiwa na mwitikio wa wananchi wanaojitokeza kwenye maonesho ya wiki ya sheria kutatuliwa changamoto zao na kupatiwa elimu juu ya masuala  mbalimbali ya kisheria.

Katibu Mkuu Maswi ameyabainisha hayo leo Januari 31,2025 Jijini Dodoma mara baada ya kutembelea mabanda ya taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za msaada wa kisheria ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya wiki hiyo yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyerere Square.

Amesema dhamira Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwa wananchi wapate huduma iliyosahihi na kwa wakati, ndiyo maana wanakutana hapo ili wafanye kazi na kutatua migogoro mingine midogo midogo na kumalizwa kwa haraka.

“Kama mgogoro ni wa kumalizika kwanini tuurushe tena na kumrudishia mtu tunatakiwa kutoa suluhisho, tumepewa nafasi hii si kwamba tuwepo tu hapana tuamuwe tufanye kazi kuisaidia Serikali yetu katika maamuzi kwa upande wa sekta hii ya sheria,”amesema.

Aidha, amewaomba wananchi waliokwenda kupata elimu katika kipindi hiki cha wiki ya sheria waiendeleze kwa wengine lakini pia pale ambapo hawajaelewa wako tayari kuwapokea na kuwaelimisha kwasababu ni wajibu waliopewa kulisaidia taifa katika eneo la sheria.

Kwa upande wake Mwanasheria Katika Wizara ya Katiba na Sheria Nuru Omari amesema katika wiki hiyo wamefanikiwa kuhudumia takribani wananchi 200 huku eneo la ardhi likionekana kuwa na changamoto kubwa.

“Katika upande huu wa ardhi tumefanikiwa kupokea takribani migogoro Kumi na ipo ambayo tumeweza kuitatua na mingine tumewapelekea Braza la Ardhi kwasababu nao wako hapa na tumepewa mrejesho,”amesema.

Moja kati ya wananchi waliotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria ni David Samson Mkazi wa Makutopora amewapongeza kwa huduma wanayoitoa na namna wanavyowahudumia wananchi hasa wale wenye changamoto mbalimbali huku akiwakaribisha wanancchi wengine kwenda kutatuliwa changamoto zao zinazowasibu.

About the author

mzalendo