Na Mwandishi Wetu – RUKWA
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amemshukuru Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoguswa na tukio la kuwaokoa Wavuvi 540 waliokuwa wanafanya shughuli za Uvuvi katika Ziwa Rukwa.
Amesema kitendo cha Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan kutoa helkopta ya Jeshi iliyoambatana na Wazamiaji wapatao 50 na vifaa maalum vya uokozi inaonesha ni jinsi gani anavyothamini maisha ya Wananchi wa Jimbo la Kwela na Mkoa wa Rukwa kiujumla.
Mhe.Sangu ametoa shukrani hizo kwa nyakati tofauti jana wakati akizungumza na Waumini wa Kigango cha Ilemba na Nankanga mara baada ya misa maalum ya kuwaombea wavuvi hao waliokumbwa na dhoruba ya upepo mkali katika ziwa Rukwa Wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa.
Amesema vikosi vilivyokuja vilisaidia
kuongeza nguvu za Uokoaji kwa kushirikiana na wananchi huku akisema vikosi hivyo visingefika kwa haraka wenda athari ingekuwa kubwa zaidi
” Mlimuona Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji CGF John Masunga walifika kuungana nasi ili kuwaokoa ndugu zetu ” amesisitiza Mhe.Sangu
Hata hiyo Mhe.Sangu amesema kwa mujibu wa taarifa ya Serikali iliyotolewa hadi kufikia jana , jumla wavuvi tisa kati ya 10 waliokuwa wanaendelea kutafutwa tangu Januari 23, 2025 wamekutwa wamefariki ambapo miili minne ilitambuliwa na ndugu zao huku miili mitano imeshazikwa kutokana hali iliyokuwa nayo.
Amewaeleza waumini hao kuwa vikosi vya uokozi bado vinaendelea na kazi ili kumpata mmoja aliyesalia huku akitoa wito kwa wananchi kuleta majina ya ndugu zao ambao hawapatikani tokea tukio hilo lilivyotokea.
Aidha, Mhe.Sangu ametoa pongezi kwa Wananchi kwa kushiriki kikamkalifu katika uokoaji pamoja na kutoa ushirikiano wa kuwatambua wavuvi wengine ambao walikuwa hawajasajiliwa katika vikundi na makampuni.
Katika hatua nyingine, Mhe.Sangu amewaeleza Waumini hao kuwa Serikali inatarajia kununua boti ya maalum ya kisasa ikayotumika katika ukanda wa Ziwa Rukwa kwa ajili ya shughuli ya uokozi wa wavuvi pale dhoruba kali ya upepo inapojitokeza.