Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Tanzania inachukulia mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika – Misheni 300 kama kichocheo cha utekelezaji wa Sera yake ya Taifa ya Nishati inayolenga kuendeleza nishati endelevu, uhifadhi na ufanisi.
Ameyasema hayo leo Januari 27, 2025 wakati akifungua Mkutano huo unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia leo Januari 27 hadi 28, 2025 ambapo majadiliano ya leo yamehusisha ngazi ya Mawaziri na Wadau wa masuala ya nishati na fedha na kesho majadiliano yatahusisha ngazi ya viongozi wakuu wa nchi za Afrika.
Mhe. Dkt. Biteko ameeleza kuwa, pamoja na maendeleo ya nishati tunayojivunia, bado nchi inahitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati kwani matarajio yake ni kukuza shughuli za kiuchumi hususan katika sekta za viwanda, madini na huduma za ukarimu jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa kimkakati zaidi katika sekta ya nishati.
Ameongeza kuwa, Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kukuza upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia barani Afrika, jitihada ambazo zimeungwa mkono na mkakati wa kitaifa na kujumuishwa katika Azimio litakalotiwa saini katika mkutano huu, huku akitoa wito wa ahadi na ushirikiano zaidi katika kuboresha upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia barani mwetu.
Aidha, amesisitiza kuwa ifikapo mwisho wa mwaka 2025, uwezo wa Tanzania kuzalisha umeme utaongezeka hadi megawati 4,000, nishati inayotoka kwenye vyanzo safi na mbadala inavyonufaisha wakazi wa vijijini na mijini, huku miundombinu ya umeme ikifikia vijiji vyote 12,318 nchini.
Pia, Tanzania inaimarisha muunganiko wa Afrika kwa kuwa na miundombinu ya umeme inayounganisha nchi za Kenya, Burundi, Rwanda, na Uganda, huku miundombinu ya kuunganisha Zambia ikiwa inaendelea.
Ametaja miongoni mwa mambo mengine yatakayofanyika katika mkutano huo kuwa ni kushirikishana uzoefu; kupata ahadi muhimu za kisiasa; kutumia ushirikiano ili kufungua uwekezaji wa sekta binafsi; kuanzisha ushirikiano wa kufadhili miundombinu ya nishati; na kukubaliana mfumo wa ufuatiliaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kiashiria cha Ufuatiliaji wa Maazimio ili kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Mkutano huo.
Ametoa rai kwa viongozi walioshiriki mkutano huo kutumia fursa hiyo kuhitimisha Maazimio yanayoendana na matarajio ya bara la Afrika ya nishati na kuimarisha ushirikiano unaohitajika katika kuyatekeleza.
“Ni matarajio yangu kwamba, mamlaka zinazohusika za nishati katika kila nchi ya majaribio zitajitahidi kuhakikisha maazimio ya nishati yanafanikishwa kupitia malengo na mipango ya hatua zinazolenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme, matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati mbadala na mchango wa mtaji wa sekta binafsi katika kufanikisha upatikanaji wa nishati”, amemalizia Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia (WB), Bw. Ajay Banga amesema kuwa bara la Afrika linaweza kubadilisha sura ya Afrika kwa kuwa na juhudi za pamoja za kuunganisha rasilimali zilizopo kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi Afrika ifikapo 2030
Nae Rais wa Benki ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi Adesina ameipongeza nchi ya Tanzania kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya vizuri katika uwekezaji wa miundombinu ya umeme kwa kuwafikishia nishati ya umeme wananchi katika vijijini vyote 12,318.
Mkutano huo umewakutanisha Mawaziri wa Nishati, Viongozi wa Taasisi za Kimataifa za Kifedha, Wataalam na Wadau wa Mashirika ya Kiraia ambao watapata fursa ya kujadili na kukubaliana malengo, vipaumbele vya sera, suluhisho, na ahadi za jinsi ya kutekeleza Mpango wa Mission 300.