Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
Waziri wa katiba na sheria Dkt.Damas Ndumbaro amefungua mafunzo ya Utawala bora na Uraia kwa viongozi mbalimbali kutoka tasisi za serikali Mkoani Kigoma yanayohusu Utawala bora na Uraia kwa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa huo.
Waziri Ndumbaro amefungua mafunzo hayo baada ya kufanya shughuli mbalimbali zilizofanyika mkoani humo ikiwemo kufungua kampeni ya huduma za msaada wa kisheria iitwayo “Mama Samia Legal Aid Campaign” katika mikoa minne ya Kigoma, Katavi, Tabora, na Mtwara.
Akizungumza katika kikao hicho Dkt.Ndumbaro amesema kuwa wizara ya katiba na sheria inamchango mkubwa katika nchi na kuifanya nchi kuwa na Amani kwa kutatua migogoro katika Jamii.
Hata hivyo Dkt.Ndumbaro amewataka viongozi hao wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kuhakikisha wanatatua migogoro mbalimbali inayowakabili wananchi kuanzia ngazi ya Vitongoji ikiwemo migogoro ya ndoa na Ardhi.
“Sisi kama viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji,mitaa,kata,wilaya na mkoa tuna jambo la kufanya na bahati nzuri kwenye ardhi tuna kamati ya vijijini inayosimamia ardhi,kwenye kata pia tuna fanya hivyo kwa hiyo niwaombe shughulikieni changamoto hiyo”
Aidha Dkt.Ndumbaro amewetaka viongozi hao kutoa elimu ya uraia kwa wananchi, uzalendo pamoja na utawala bora kuwa ni utawala wa sheria na unaotenda haki.
Sanjari na hayo pia Dkt. Ndumbaro, amewataka wananchi kutimiza wajibu wao kwa kuchangamkia fursa ya kupokea elimu na huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa kupitia kampeni hiyo.
Kampeni hiyo itafanyika kwa siku 9 mfululizo katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuwafikia wananchi na kuwawezesha kupata haki zao za kisheria kwa urahisi.