NA MWANDISHI WETU, OR-TAMISEMI
Zaidi ya wadau wa afya 2500 kutoka nchi 25 duniani wanatarajiwa kushiriki kongamano la masuala ya afya hapa nchini (Tanzania Health Summit) litakalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 1 hadi 3, 2025.
Hayo yameelezwa Januari 24, 2025 jijini Dodoma na Rais wa Tanzania Health Summit Dkt. Ommary Chillo katika mazungumzo yake na Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kongamano hilo pamoja na masuala mengine ya OR – TAMISEMI kupitia Idara ya Afya ambapo italitumia jukwaa hilo kufanya mjadala kuelezea vipaumbele vyake upande wa sekta ya afya kwa mwaka 2025.
Dkt.Chillo amesema kongamano hilo litaenda sambamba na mabanda ya maonesho zaidi ya 100 pamoja na kusomwa au kuwasilishwa kwa zaidi ya ripoti 250 za utafiti wa masuala ya afya.
Pia, ametumia fursa hiyo kuwasilisha ripoti ya mkutano wa 11 uliofanyika Oktoba 1 hadi 3,2024 visiwani Zanzibar ambao ulijikita kuangalia ubia kati ya sekta binafsi na ya umma unavyoweza kuboresha ubora wa huduma za afya nchini.