Featured Kitaifa

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA WIZARA UTEKELEZAJI PROGRAMU KIZAZI CHENYE USAWA, UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI

Written by mzalendo

Na WMJJWM-Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuratibu kwa ufanisi utekelezaji wa Programu ya Tanzania ya Kizazi chenye Usawa (GEF) na Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF).

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatma Toufiq wakati wa uwasilishaji wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Januari 22, 2025 jijini Dodoma.

Mhe Toufiq amesema Wizara imekuwa nguvu kuhakikisha jamii inapata maendeleo kupitia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali katika sekta mbalimbali nchini jitihada hizo zinasadia kutatua changamoto za wananchi na kuwainua kiuchumi.

” Wizara mnafanya kazi kubwa sana kuhakikisha jamii inapata maendeleo na ustawi, tunaiona kazi yenu Kamati itaendelea kuwaunga mkono ili kufikia maono ya Rais ya kuanzisha Wizara hii ya mambo ya maendeleo na ustawi wa jamii” amesema Mhe.Toufiq

Akiwasilisha taarifa mbele ya Kamati hiyo ya Bunge, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Wizara itaendelea kuratibu utekelezaji wa Programu mbalimbali kuhakikisha zinafikia malengo yake na kuunga mkono jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo na kuboresha ustawi wa wananchi.
Aidha Waziri Dkt. Gwajima ameishukuru Kamati hiyo kwa kutoa ushirikiano na maelekezo yanayosaidia Wizara kusonga mbele katika kutekeleza Sera na Programu mbalimbali.

Akitoa ufafanuzi ya hoja zilizojitokeza mbele ya Kamati hiyo, Kaimu Katibu Mkuu Wakili Amon Mpanju amesema katika kuimarisha huduma kwa jamii hasa kwa Watoto na Wazee, Wizara itashirikiana na Mamlaka ya Mikoa na Serikali za Mitaa ili kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kuwekeza katika huduma hizo.

About the author

mzalendo