Featured Kitaifa

TANZANIA MWENYEJI WA MKUTANO WA TATU WA NCHI ZINAZOZALISHA KAHAWA AFRIKA

Written by mzalendoeditor

 

WAZIRI wa kilimo Mhe.Hussein Bashe,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Januari 14,2025 jijini Dodoma kuelekea  mkutano wa tatu  wa  nchi zinazozalisha kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit) unaotarajiwa kufanyika Februari  21 na 22 mwaka huu  jijini Dar es  Salaam.Kushoto ni Naibu Waziri Mhe.David Silinde.

WAZIRI wa kilimo Mhe.Hussein Bashe,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati akizungumza  kuelekea  mkutano wa tatu  wa  nchi zinazozalisha kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit) unaotarajiwa kufanyika Februari  21 na 22 mwaka huu  jijini Dar es  Salaam.Kushoto ni Naibu Waziri Mhe.David Silinde.

WAZIRI wa kilimo Mhe.Hussein Bashe,akizundua  mkutano wa tatu  wa  nchi zinazozalisha kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit) unaotarajiwa kufanyika Februari  21 na 22 mwaka huu  jijini Dar es  Salaam.  

Na.Alex Sonna-DODOMA

RAIS  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi  katika Mkutano wa tatu  wa  nchi zinazozalisha kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit) uliopangwa kufanyika February 21 hadi 22,mwaka huu kwenye  ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere  jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Januari 14,2025 jijini Dodoma na Waziri wa kilimo Mhe.Hussein Bashe,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo ambao umeandaliwa kwa  kushirikiana na Shirika la Kahawa la Afrika (IACO) kauli mbiu ya  Mkutano huo ni “Kufungua Fursa za Ajira kwa Vijana Kupitia Uboreshaji wa Sekta ya  Kahawa Afrika.” .  

Bashe amesema  mkutano huo utahudhuriwa na Wakuu wa nchi zinazolima Kahawa Barani Afrika,  Mawaziri wa Kilimo, Sekta Binafsi, Viongozi wa Taasisi za Kahawa katika nchi zinazolima  Kahawa, Wakulima na Wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa Kahawa.

“Mkutano huu utatoa mwongozo wa jinsi ya kushirikiana na Umoja wa Afrika na Mashirika yake, Benki za Maendeleo za Afrika na taasisi nyingine za fedha ili kuunda programu zinazochochea  ujasiriamali na ajira kwa vijana kupitia Sekta ya Kahawa.”amesema Mhe.Bashe

Amesema  lengo la Tanzania kuomba uwenyeji wa mkutano huo ni pamoja na kutaka kuwaelewesha watanzania juu ya umuhimu wa zao la Kahawai hapa nchini na duniani kote,lakini kushawishi wakulima wajikite katika kilimo hiko.
Bashe amesema kuwa uzalishaji wa zao la Kahawa hapa nchini umeongezeka kutoka tani 34,000 hadi kufikia Tani 85,000 kwa mwaka jana,ambapo alisema  hiyo ni hatua kubwa katika kilimo cha zao hilo.
“Serikali iko katika hatua za kuliongezea mnyororo wa thamani wa zao hilo,ndio maana wameandaa mkutano huo ili wadau wa sekta ya Kahawa kuja.kubadilisha mawazo kuhusu zao hilo lakini pia kuona umuhimu wa biashara hiyo dunianie”amesema Bashe .
Aidha amesema kuwa Kituo cha Utafiti wa zao la Kahawa  kwa nchi za Afrika kinatarajia kujengwa mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kufanyia utafiti zao hilo kabla ya kuingia sokoni
Kuhusu ujenzi wa kituo cha Utafiti cha Kahawa ambacho kitafanya kazi ya utafi,Bashe alisema 
walikubaliana na Taasisi ya Uzalishaji Kahawai Afrika (IACO),kutoa eneo kwa ajili kituo kikubwa cha utafiti wa zao la Kahawa barani ambacho kitajengwa mkoani Kilimanjaro.
Amesema wameiomba Taasisi ya Uzalishaji Kahawai Afrika (IACO) kushirikiana nao kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho ili kuhakikisha Kahawa inayozalishwa Barani Afrika ikiwemo Tanzania inakuwa safi.

Ameongeza kuwa kwa upande wa Tanzania utekelezaji huu umeanza kupitia Wizara ya Kilimo ambapo  imezindua programu wa ujasiriamali kwa vijana uitwao Jenga Kesho Iliyo Bora – Build a  Better Tomorrow – BBT ambapo mojawapo ya mipango inayotekelezwa ni kuanzisha  “Maduka ya kahawa yanayotembea” ili kuchochea na kuongeza matumizi ya kahawa nchini,”

 

Hata hivyo Mhe.Bashe  amesema mpango wa kuanzisha mkutano wa nchi wazalishaji wa kahawa Afrika ni matokeo ya azimio  lililopitishwa wakati wa mkutano wa 61 wa mwaka wa IACO uliofanyika Kigali, Rwanda, Novemba 18, 2021, la kuandaa mkutano wa ngazi ya juu wa nchi 25 zinazozalisha kahawa  barani Afrika ili kutathmini mapungufu na changamoto zinazosababisha kudumaa kwa wa sekta  ya kahawa Barani Afrika. 

“Baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Mkutano wa kwanza wa nchi wazalishaji wa kahawa  Afrika ulifanyika nchini Kenya mwezi Mei 2022, na ulipitisha “Tamko la Nairobi” (Nairobi  Declaration) ambalo liliazimia kuweka mkakati wa kuingiza zao la kahawa kama bidhaa  muhimu ya kimkakati katika Umoja wa Afrika (AU) sambamba na Agenda 2063 ya AU.”amesema Mhe.Bashe

Aidha  amesema  mkutano wa pili wa nchi wazalishaji wa kahawa Afrika uliofanyika Kampala, Uganda, Agosti  2023, ulipitisha Tamko la Kampala (Kampala Declaration) ambalo lilikusudia kuwaomba Wakuu wa Nchi 25 zinazozalisha kahawa barani Afrika kuunga mkono kuidhinishwa na  kujumuishwa kwa zao la kahawa kama bidhaa muhimu ya mkakati katika AGENDA 2063 ya  AU na kuifanya IACO kuwa shirika maalum la Umoja wa Afrika.

Katika Kikao cha 37 cha kawaida cha Baraza la kuu la umoja wa Afrika kilichofanyika Februari  2024 huko Addis Ababa, Wakuu wa Nchi na Serikali walipitisha kwa kauli moja kuingiza zao la  kahawa kama bidhaa muhimu ya mkakati katika AGENDA 2063 ya AU na kuifanya IACO kuwa  shirika maalum la Umoja wa Afrika. 

Amesema kuwa moja ya hatua zilizochukuliwa katika kutatua changamoto za biashara ya kahawa baina ya nchi  za Afrika ni kuanzishwa kwa Mkataba wa Biashara Huria Afrika (African Continental Free Trade  Area – AfCFTA) wa 2018 kwa lengo la kuondoa vikwazo vya biashara katika ya nchi za Africa na  hivyo utekelezaji kamili wa mkataba huo utaimarisha biashara ya kahawa bila vizuizi baina ya  nchi za Africa.

Hivyo, Mkutano huu wa Tatu  utajadili maeneo muhimu katika mnyororo wa  thamani wa kahawa kwa ajili ya kufungua fursa za biashara na ajira kwa vijana. 

About the author

mzalendoeditor