Featured Kitaifa

MHE. NDERIANANGA AKABIDHI MISAADA WAATHIRIKA MAFURIKO SAME

Written by mzalendo

Na Mwandishi wetu- Kilimanjaro

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kutenga bajeti kwa ajili ya kukabiliana na maafa yanapotokea pamoja kutambua maeneo hatarishi.

Mhe. Nderiananga alitoa kauli hiyo wakati akikabidhi misaada ikiwemo mahindi tani 3.2, ndoo 25, madumu 25, vikombe na vijiko kwa waathirika wa mafuriko wa Kata za Bombo, Msindo, Vuje, Mtii na Maore wilayani Same ambapo jumla ya watu sita walifariki Dunia kwa kuangukiwa na ngema katika nyumba zao.

Alisema kuwa, kuwepo kwa bajeti hiyo kunasaidia kuwahudumia waathirika wa maafa mara pale inapotokea, hali ambayo itasaidia kurejesha tabasamu kwa waathirika wakati wanapoendelea kusubiri msaada kutoka Serikali kuu.

“Halmashauri sasa mnawajibu wa kuhakikisha katika bejeti yenu mnatenga fedha kwa ajili ya kukabiliana na maafa pindi yanapotokea ili muwahi mapema na kuwasaidia wahanga kwa haraka lakini yapo maeneo ambayo ni hatarishi maafa yamekuwa yakijirudiarudia mnapaswa kuyatambua na kuwaelimisha wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuhama,” alisema Mhe. Nderiananga.

Aidha, ameitaka halmashauri, kuandaa mipango ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko pamoja na kuimarisha vifaa vya uokozi ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza pamoja na kuyatambua maeneo yote hatarishi na kuanza kuwaelimisha wananchi kuhama katika maeneo hayo ili kuepuka madhara mbalimbali yanayoweza kutokea.

Katika hatua nyingine alibainisha kwamba, Serikali inashughulikia changamoto ya upatikanaji wa mbegu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuhakikisha wananchi walioharibikiwa mazao yao wanapata mbegu za mahindi na mpunga haraka kurejesha mazao ambayo yamesombwa na maji ili kuepukana kuibuka kwa janga la njaa hapo baadaye.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Same Bi. Kasilda Mgeni alisema kuwa, katika mafuriko hayo watu 10 wamepata madhara ambapo kati yao watu sita walifariki Dunia kutokana na kuangukiwa na vifusi katika nyumba zao, nyumba 34 zimeharibika, hekari 260 za mazao zimeharibika na miundombinu ya barabara ambapo kwa sasa Serikali inaendelea na juhudi za kurejesha mawasiliano.

“Tumewaagiza wakala wa Barabara TANROAD kuhakikisha mlango wa daraja la Komwex linalounganisha Kijiji cha Maore na Mheza kupanuliwa ili kuwezesha magogo na takataka za mashambani kupita kwa urahisi na kutosababisha maji kupita juu ya Daraja,” alisema Bi. Kasilda.

Naye Katibu wa Mbunge wa Same Mashariki, Bw. Semu Mmamba alieleza kwamba watu wanaoishi milimani maeneo yao yameharibika na mengine yanasogea na hivyo kuleta athari milimani na bondeni.

“Nashukuru sana kwa jitihada zilizofanywa na Serikali kwa kupitia Kamati za Maafa kwa kazi nzuri iliyofanywa ya kuratibu na kuwafikia wahusika ikiwa ni pamoja na kutoa msaada kwa haraka,” alieleza.

Aidha, Diwani wa Kata ya Maore Bwa. Rashid Juma alisema, “Mifereji yetu mingi imeharibiwa na mvua tunaiomba serikali itume wataalam wake kuja kurejesha mifereji yetu hii pamoja na kutupatia mbegu turejee mashambani kulipa hiki ndio kilio chetu kikubwa maana hata mkitupa chakula leo kitaishi na tutarudi kulekule kwenye kuomba lakini tukirejea mashambani tutajitegemea wenyewe”.

About the author

mzalendo