Ofisi ya Uchunguzi wa Maafisa wa Ngazi za Juu (CIO) ilithibitisha kutolewa kwa waranti wa kumkamata Yoon siku ya Jumanne na Mahakama ya Wilaya ya Seoul Magharibi iliyoombwa na wachunguzi wanaochunguza sheria ya kijeshi iliyodumu kwa muda mfupi.
Yoon, ambaye kwa sasa amesitishwa kazi na bunge, anakabiliwa na uchunguzi kutokana na tuhuma kwamba alikuwa kiongozi wa uasi, mojawapo ya mashitaka ya uhalifu ambayo rais wa Korea Kusini hana kinga nayo.
Waranti huo wa kukamatwa kwa Yoon unaweza kutumika hadi tarehe 6 Januari na unawapa wachunguzi masaa 48 tu ya kumshikilia mwanasiasa huyo baada ya kumkamata. Baada ya hapo, wachunguzi wanapaswa ama waranti ya kumuweka kizuizini ama kumuachilia.
Mara tu akitiwa nguvuni, Yoon anatazamiwa kuwekwa kwenye Kituo cha Kuzuilia Watuhumiwa cha Seoul, kwa mujibu wa shirika la habari la Yonhap ambalo liliinukuu ofisi ya CIO.
Hata hivyo, wakili wa kiongozi huyo, Yoon Kab-keun, alisema waranti ya kumkamata mteja wake ulikuwa haramu na ulio kinyume na sheria kwa sababu CIO haikuwa na mamlaka kuomba waranti huo kwa mujibu wa sheria za Korea Kusini.
“Timu yetu ya wanasheria itawasilisha zuio kwenye Mahakama ya Katiba kuzuwia waranti huo,” aliongeza wakili huyo.
Imeandikwa na Idhaa ya Kiswahili ya DW.