Featured Kitaifa

ATAKAYEBADILISHA MATUMIZI YA FEDHA ZA MIRADI NA KULIPA POSHO ATACHUKULIWA HATUA’ DKT. GRACE

Written by mzalendoeditor

Na. James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe amesema Serikali itachukua hatua dhidi ya viongozi wa Halmashauri watakaobainika kulipa posho za watumishi kwa kutumia fedha ambazo zimetengwa na Serikali kwa ajili ya kununua bidhaa za afya ili kuboresha utoaji huduma za afya msingi nchini.

Dkt. Magembe amesema hayo katika Ukumbi wa Ngome Saccos jijini Dar es Salaam, wakati akifungua kikao kazi cha wadau chenye lengo la kujadili uboreshaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na huduma muunganisho za Afya tarehe 16.12.2024.

“Nimepita katika halmashauri zenu na kubaini vifungu ambavyo vilikuwa vinalipia bidhaa za afya vimelipia posho, hizo ni hoja za ukaguzi hivyo mtachukuliwa hatua na CAG, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Afya,” Dkt. Magembe amesisitiza.

Dkt. Magembe amewahimiza washiriki wa kikao kazi hicho kuzingatia miongozo ya matumizi sahihi ya fedha za bidhaa za afya na kuongeza kuwa, kama kiongozi au mtumishi anaona kuna ulazima wa kubadili matumizi ya fedha za bidhaa za afya ni vema akasubiria muda wa kubadili matumizi ya fedha (reallocation) ufike ili mabadiliko yafanyike kwa mujibu wa taratibu.

“Wafamasia wa mikoa, wataalam wa maabara wa mikoa na waratibu wa afya wa mikoa mliopo hapa ni wazi kuwa zoezi la kubadili matumizi ya fedha iwapo kuna ulazima ni jukumu ambalo mnapaswa kulitekeleza wakati wa kipindi cha kubadili matumizi ya fedha (budget reallocation),” Dkt. Magembe amehimiza.

Sanjali na hilo, Dkt. Magembe amefafanua kuwa, kitendo cha kubadili matumizi ya fedha za afya bila kuzingatia utaratibu kinapekea kuibuka kwa migogoro isiyo ya lazima pindi unapofika wakati wa kulipia bidhaa hizo MSD au kwa mshitiri kwani kifungu husika kinakuwa kimeshatumika kulipia posho au huduma nyingine ambazo haziusiani na bidhaa za afya.

About the author

mzalendoeditor