Featured Kitaifa

MAVUNDE AWAKABIDHI NYUMBA WATOTO WALIOMPOTEZA MAMA YAO KWA KUFUNIKWA NA KIFUSI

Written by mzalendoeditor
Na.Alex Sonna-DODOMA
MBUNGE wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde amekabidhi nyumba ya kisasa kwa watoto Hamis na Baraka ambao waliachwa na Mama yao ambaye alifariki kwa kufunikwa na kifusi  mara baada ya kuangukiwa na nyumba.
Mwaka jana katika Mtaa wa Nguji -Kata ya Mbabala Jijini Dodoma watoto hao waliachwa peke yao mara baada ya Mama yao kudondokewa na nyumba na kupoteza maisha na hivyo kuachwa wakiwa hawana makazi kutokana na athari ya mvua zilizokuwa zikinyesha.
Kutokana na Hali hiyo,Mhe.Mavunde  aliahidi kuwajengea nyumba pamoja na kuwapatia huduma muhimu ikiwa pamoja na kuwapeleka shuleni kwa ajili ya kuwasomesha kwa gharama zake mwenyewe.
Mapema Leo Desemba 9,2024 Mavunde ameitekeleza ahadi hiyo kwa vitendo kwa kuwakabidhi nyumba,vitanda,makabati pamoja na vifaa vya shule watoto hao.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Mavunde amesema alipokutana na jambo hilo mwaka jana alisikitika na kuahidi kuwajengea nyumba pamoja na kuwapa mahitaji muhimu.
“Namshukuru Mungu nimeweza kukamilisha ujenzi  wa nyumba kupitia nyumba hii watakuwa salama na uwepo wa nyumba hii utawasaidia.Nilienda mbali baada ya kupatikana kwa nyumba nimesaidia pia upatikanaji wa vitanda na magodoro ambapo awali walikuwa hawana na makabati ya kuhifadhi nguo pamoja na vifaa vya shule kwani awali niliahidi kuwasomesha na nimewaletea na vyakula vya kuanzia,”amesema Mavunde
Hata hivyo amesema anaamini watasimamiwa vizuri na wahusika ili waweze kutimiza ndoto zao ambazo zilianza kupotea mara baada ya kumpoteza Mama yao.
Aidha,Mhe. Mavunde amesema Kata ya Mbabala ni mlezi wa kituo cha watoto yatima ambao amekuwa akiwahudumia hivyo amewaomba wahusika wa kituo hicho kuwasaidia kimaadili watoto hao.
Kwa upande wake mtoto Hamis,amemshukuru Mbunge huyo kwa kuwasaidia kupata nyumba bora ambayo wataishi.
“Tunamshukuru Mhe.Mavunde kwa moyo wake wa kutujengea hii nyumba tunashukuru Sana ulivyotujengea nyumba tunakuombea kwa Mungu uendelee na moyo huo wa kutusaidia,”amesema mtoto huyo.
Naye,Diwani wa Kata ya Mbabala  Mhe. Pascazia Mayala,amesema Mbunge huyo anafanya mambo  ya  kipekee ambayo wanamshukuru kwa kuitekeleza kwa vitendo ilani ya CCM.
Amesema nyumba hiyo ni kielelezo cha Mbunge hiyo kutekeleza kwa vitendo ahadi zake na wanamuomba Mwenyezimungi azidi kumbariki.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini Mhe.Mavunde katika Nafasi ya Waziri wa Madini kwani anaitendea haki kwa vitendo.”amesema Mhe.Mayala
Awali Mlezi wa familia hiyo na Mchungaji wa DCT Mbabala Lazaro Ijinji,amesema wanamshukuru Mavunde kwa kazi kubwa anayofanya na moyo wake wa kizalendo kwani anazidi kufanya mambo makubwa  ambayo yanagusa jamii.
“Naaamini kama angetoa fedha ingekuwa imeisha lakini ameamua kutoa nyumba na fenicha tunashukuru Sana kwa tendo hili umetupa pa kusimamia kwa matendo yako makubwa,”amesema

About the author

mzalendoeditor