Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Raisi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) Mhe. Imani Daud Aboud leo Novemba 04, 2024 ametembelea Makao makuu ya ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) yaliyopo Mkoani Dodoma kwa lengo la kufanya mazungumzo na Uongozi wa tume hiyo na kuifahamisha majukumu na ya Mahakama hiyo.
Akielezea mamlaka hiyo Mhe. Aboud amegusia suala la Tanzania kujiondoa katika tamko linaloruhusu Mahakama kupokea Mashauri yanayopelekwa na Wananchi au mashirika yasiyo ya kiserikali.
Mhe. Aboud amesema kuwa THBUB ni mdau muhimu katika kuhakikisha dhumuni la kuanzishwa kwa Mahakama linatimizwa ikiwa ni pamoja na kulinda haki za Binadamu.
“THBUB inapaswa kujihusisha na huu mchakato wa kuona kwamba Tanzania inaweka mkazo suala la kurudisha hilo tamko ili kuwaruhusu watanzania waweze kupata huduma za mahakama yao kwani Mahakama ya Afrika ni mahakama ya waafrika wote na Nchi zote za umoja wa Afrika zinachangia fedha kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za Mahakama hiyo” amesema Mhe. Aboud.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa THBUB Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu) amesema kuwa zipo changamoto zilizosababisha Tanzania kujitoa na Tume inaona kuwa changamoto hizo zinaweza kutatuliwa na Tanzania ikaweza kurudisha tamko hilo ili wananchi waweze kunufaika na Mahakama hiyo.
Aidha Mhe. Mwaimu amesema kuwa Serikali imekuwa inatoa gharama nyingi katika kuhakikisha mahakama hiyo inaendelea kufanya kazi zake hivyo bado kuna fursa ya Serikali kurudisha tamko hilo ili watanzania waendelee kufurahia huduma hizo.
“Mahakama hii na Serikali ya Tanzania zinaweza kukaa kwa pamoja na kutatua changamoto zilizopo na kuweza kurudisha tamko hilo la kuruhusu wananchi Kwenda katika mahakama hiyo” amesema Mwenyekiti wa THBUB.
Katika ziara hiyo Rais Aboud aliambatana na Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo Mhe.Modibo Sacko na Mhe. Jaji 8Duncan Gaswaga pamoja na watendaji wengine wa Mahakama.
Tanzania iliandika kusudio la kujiondoa katika tamko hilo Novemba 2020 katika ibara ya 34 (6) ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ambayo inaruhusu watu binafsi na asasi zisizo za kiserikali kuwasilisha mashauri ya Haki za Binadamu.