Featured Kitaifa

CHUO CHA DTI KITAENDA KUENDELEZA NA KUKUZA BUNIFU ZA WATANZANIA : SILAA

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema ili kuchochea ukuaji wa Sekta ya TEHAMA nchini imedhamiria kujenga Chuo mahiri cha TEHAMA (DTI) katika eneo la Nala mkoani Dodoma ili kuendelea kukuza bunifu za Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 5,2024 Jijini Dodoma, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa amesema Chuo hicho kitakuwa kituo muhimu cha kuboresha Bunifu mbalimbali zinazozalishwa na Watanzania na kuwasaidia kuingia sokoni.

“Kwahiyo chuo hiki kitakuwa na kazi ya kuwachukua vijana wale wenye bunifu zao walioko mtaani kuweza kuwasaidia bunifu zao kuwa tija na kufuata sheria, kwa mfano unakuta kijana anafanya ubunifu kumbe ule ubunifu wake ni kinyume cha sheria lakini kwaakili yake anaona ule ubunifu uko vizuri sasa hatua hii itaweza kuwasaidia pakubwa wabunifu wetu, “amesema.

Sambamba na hayo ameongeza kuwa kazi nyingine ya chuo hicho itakuwa ni kuwaunganisha wadau mbalimbali na zile bunifu ili wapate sehemu ya kufanyia majaribio na ikitoka pale iwe bidhaa inayouzika lakini vilevile na taasisi kubwa za ndani na nje ya nchi zinazohitaji bunifu hizo zipate sehemu ya kufikia.

Pia ameelezea hatua ambayo tayari zimeshafanyika kuelekea ujenzi wa Chuo hicho ikiwemo upembuzi yakinifu, ambapo amesema ujenzi huo utakamilika ndani ya miaka miwili.

“Tayari yapo mambo ambayo yamekamilika ambapo Serikali au Wizara imepata eneo kule Nala hekari 400 na hati tunayo ipo chini ya Katibu Mkuu wa Wizara na ujenzi utakapokuwa umekamilika kwa miaka miwili ndipo tutaanza kuona matunda sasa,”ameeleza.

Ujenzi wa chuo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa tatu wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2021/2026 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 ambayo inasisitiza uwepo wa mafunzo ya Ujuzi na Ubunifu katika TEHAMA nchini.

About the author

mzalendo