Na. Na Mwandishi wetu, Dodoma
Mkurugenzi wa Shirika la Bridge for Change Bw. Ocheki Msuva ambaye ni mtaalamu wa Siasa na Utawala anayejiushisha na masuala ya vijana katika eneo la ushiriki na ushirikishwaji amesema, uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeisha hivyo ni muhimu kufunguka kwa majukwaa ya mazungumzo na majadiliano yenye kujenga umoja wa kitaifa kwa maslahi ya maendeleo ya taifa.
Bw. Msuva ametoa wito huo leo jijini Dodoma, ikiwa ni siku ya nne mara baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa kutangaza matokeo ya jumla ya uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024.
Bw. Msuva ameanisha kuwa, muda huu ni wakati muafaka wa kufunguka kwa majukwaa ya mazungumzo na majadiliano yenye kujenga jamii moja ili kutoa fursa ya kuwasikiliza wale ambao wanaona kwa namna moja au nyingine hawakulizika na mchakato wa uchaguzi, fursa hiyo itakuwa ni sehemu ya kufanya maboresho kwa mustakabali wa uchaguzi ujao.
“Ushauri wangu kwa vyama vya siasa na wananchi ambao wanaona kulikuwa na dosari chache katika mchakato wa uchaguzi, ni muhimu wakawa ni sehemu ya kutoa maoni ya kiulijenga taifa ili kujiepusha na athari zitakazolikwamisha taifa kupiga hatua katika maendeleo,” Bw. Msuma amesisitiza.
Sanjali na hilo, Bw. Msuva amehimiza kuwa uchaguzi huu umekuwa wa kipekee sana kwani unatoa fursa ya kutafakari kama jamii, ni kwa namna gani tunataka kusonga mbele na kuwa sehemu ya mabadiliko katika kuchagiza maendeleo ya taifa letu,” Bw. Msuva amehimiza.
Bw. Msuva ameongeza kuwa, huu ndio wakati wa kushikamana, kujadiliana, kujenga umoja na kufikiri ni kwa namna gani bora zaidi tunaweza kuwa ni sehemu ya mchakato wa maendeleo bila kuvunja umoja wetu na amani tuliyonayo katika taifa.
Aidha, Bw. Msuva amesema ni wazi kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024 kwa kiasi kikubwa umefanyika kwa amani na utulivu na ndio maana wananchi wengi wameshiriki tofauti na chaguzi zilizopita ambazo hazikuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi.
“Kitendo cha wananchi wengi kujitokeza kupiga kura kinaashiria kwamba walipewa hamasa na elimu ya kutosha, hivyo walipata mwamko wa kutambua wajibu wao kikatiba na umuhimu wa kupiga kura,” Bw. Msuva amesisitiza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwaongoza watanzania 26,963,182 kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024.