Wanawake nchini wameendelea kuhamasishwa kuchangamkia fursa zitokanazo na nishati safi ya kupikia zikiwamo za utengenezaji wa majiko banifu na mkaa mbadala.
Rai hiyo imetolewa leo mkoani Dar es Salaam na Mtaalam wa Jinsia na Nishati kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Joseph Sambali wakati akitoa mada kuhusu nishati safi ya kupikia katika Kongamano la mafunzo ya ujasiriamali, uwekezaji na matumizi ya nishati safi.
Kongamano hilo lilolowakutanisha wanawake wajasiriamali kutoka Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Dar es Salaam lilikuwa limeandaliwa na Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya ALSF.
βKatika kuendelea kutekeleza kwa vitendo Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi wa Kupikia na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sisi kama REA tunafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha ifikapo 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Ili kufikia lengo hilo, tumeanza kuwafikishia wananchi mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku ambapo mitungi zaidi ya 400,000 itagaiwa. Tunatarajia pia kugawa majiko banifu zaidi ya 200,000 kwa bei ya ruzuku. Tungependa kuendelea kuwahamasisha wanawake kuchangamkia fursa zikiwamo za kutengeneza majiko banifu au mkaa mbadala pamoja na fursa mbalimbali zilizopo kupitia utekelezaji wa mkakati wa nishati safi ya kupikia.β Amesema Dkt. Sambali.