Featured Kitaifa

KITIVO CHA UONGOZI WA BIASHARA OUT CHAASWA KUTOA ELIMU YA UJASIRIAMALI

Written by mzalendoeditor

Kitivo cha Uongozi wa Biashara katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimehimizwa kuendelea kutoa elimu ya ujasiriliamali ambayo itasaidia vijana na makundi mbali mbali katika jamii kuweza kujiajiri na kuondokana na dhana ya kusubiri kuajiriwa pale wanapomaliza masomo yao ya chuo kikuu.

Akifungua mdahalo wa kitaaluma katika kuadhimisha miaka 30 ya OUT uliokuwa na mada “Miaka 30 ya Elimu ya Biashara kupitia Mifumo Huria, Masafa na Mtandao: Kuunganisha Kisomo na Uajirikaji”, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Leonard Fweja, ambaye ni Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo wa Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa, amepongeza uwepo wa Mdahalo huu kwani ni mojawapo ya fursa ya kujadili na kubadilishana uzoefu, na utatuzi wa changamoto ambazo zinakwamisha utekelezaji wa majukumu fulani katika kitivo.

“Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inabadili mtazamo wake wa elimu kutoka katika elimu ya nadharia kwenda zaidi katika vitendo halisi ili kumwezesha mtu kuweza kufikiri kujiajiri pindi anapomaliza masomo yake. Kwa elimu ya ujasiriamali tunayoitoa itamwezesha mkulima kupata elimu ya usindikaji wa kuchakata mazao yake hivyo atayahifadhi kwa muda mrefu na hii itakuwa ni faida kwa mfanyabiashara huyo na katika sekta nzima ya uwekezaji kwenye taifa letu kwani atatumia maarifa hayo katika kuendesha biashara yake,” amesema Prof. Fweja.

Ameongeza kwa kufafanua “Tuna wahitimu wengi wameweza kutumia hiyo elimu kuweza kuanzisha miradi mbalimbali katika jamii, mfano kuna mmoja ameanzisha miradi mbalimbali katika mkoa wa Njombe, na mwingine ametoka magereza ameweza kuanzisha miradi mbalimbali kule na kuchochea elimu ya ujasiriamali katika kazi zake kwahiyo wanafunzi wetu wengi wamemaliza chuo na kufanya mambo mengi mazuri kwa kujiajiri zaidi kuliko kuajiriwa”.

Prof. Lemayon Melyoki kutoka Shule Kuu ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) amesema, OUT imeongeza fursa za watu kuweza kupata elimu ya ujasiriamali na imetoa watu wengi sana ambao wameweza kuingia katika jamii kufanya kazi mbalimbali katika serikali pamoja na sekta binafsi. Elimu ya ujasiriamali inasaidia sana vijana kuweza kutafuta namna ya kujiajiri pale wanapohitimu elimu. Hili ni mojawapo ya suluhu kwa serikali katika kukabiliana na tatizo la ajira nchini.

Naye Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, Dkt. Tumaini Katunzi akiwasilisha mada katika kongamano hilo amehimiza matumizi ya Data Kubwa “BIG DATA” kwa OUT ikiwa kama taasisi inayofundisha na kutoa wakufunzi katika biashara, hii itasaidia katika kufanikisha malengo yake makuu hasa katika data za wanafunzi, data za mitihani na data za kufundishia na kufanya maamuzi sahihi baada ya kupitia mkusanyiko wa data hizo.

Mkuu wa Kitivo cha Uongozi wa Biashara OUT, Dkt. Joseph Magari ameeleza namna OUT inajivunia kutoa wahitimu waliotumia elimu ya ujasiriamali kuweza kufanikisha mambo yanayohusiana na ajira katika maeneo yao wanayofanyia kazi.

“kwa sasa tupo katika mchakato wa kuhuisha mitaala na tunalenga kubadilisha mitaala ili kumfikirisha mtu kujiajiri kuliko kuajiriwa, kwa sasa somo la ujasiriamali tunalo na lipo katika nadharia na vitendo kwahiyo katika mchakato unaoendelea wa kuhuisha mitaala yetu tutaweka kipaumbele katika kuboresha dhana ya kujiajiri kuliko kuajiriwa.

Mdahalo huu ni muendelezo wa matukio ya Maadhimisho ya Miaka 30 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambapo kilele chake kinatarajiwa kuwa katika Mahafali ya 43 ya chuo hiki mkoani Kigoma.







About the author

mzalendoeditor