KATIBU Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU),Prof. Charles Kihampa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Oktoba 4,2024 jijini Dodoma kuhusu kuongeza muda wa udahili kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika programu ambazo bado zina nafasi kwa mwaka wa masomo 2024/2025 unaotarajia kuanza kesho Oktoba tano hadi Oktoba tisa mwaka huu.
N.Gideon Gregory-DODOMA
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imeongeza muda wa udahili kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika programu ambazo bado zina nafasi kwa mwaka wa masomo 2024/2025 unaotarajia kuanza kesho Oktoba tano hadi Oktoba tisa mwaka huu.
Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa,ameyasema hayo leo Oktoba 4,2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wahabari ambapo amesema kuwa vyuo na waombaji wanapaswa kuzingatia utaratibu wa udahili awamu ya tatu.
Prof.Kihampa amesema kuwa awamu hiyo ya tatu itakuwa ya mwisho kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga masomo ya shahada ya kwanza, imefunguliwa kwa programu ambazo bado zina nafasi katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
“Baada ya kukamilika kwa awamu zote mbili za udahili, tume imepokea maombi ya kuongeza muda kutuma maombi ya udahili kutoka Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO).
“Pia, tumepokea maombi kutoka kwa baadhi ya waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika awamu zilizopita na vyuo ambavyo ambavyo vimeomba kupewa muda kuendelea kudahili,” amesema Prof.Kihampa
Aidha Prof.Kihampa ametoa wito kwa waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakuweza kupata nafasi katika wamu ya pili kutokana na sababu mbalimbali, watumie fursa hiyo kutuma maombi yao.
Katika hatua nyingine, Prof.Kihampa amesema kuwa udahili katika awamu zote mbili kwa ngazi ya shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2024/2025, umekamilika.
Amefafanua kuwa majina ya waombaji waliodahiliwa katika awamu hiyo yatatangazwa na vyuo husika kuanzia kesho.
Hata hivy0 amesema kuwa waombaji waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja katika awamu ya pili na wale ambao hawakuthibitisha udahili katika awamu ya kwanza, alisema wanapaswa kuthibitisha katika chuo kimoja kuanzia leo hadi Oktoba 21 mwaka huu.
“Uthibitisho huo utafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili,” amesisitiza Prof.Kihampa