Featured Kitaifa

PPAA YAFANYA TATHMINI YA MODULI YA KUWASILISHA MALALAMIKO/RUFAA KIELETRONIKI

Written by mzalendo

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeanza kufanya tahmini ya kutumia Moduli ya kupokea na kuwasilisha malalamiko na rufaa kieletroniki katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kieletroniki (NeST).

Kufanyika kwa tahmini hiyo ni kuashiria kuwa muda si mrefu moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko itaanza rasmi kutumika kama ilivyokuwa imekusudiwa.

Akifungua kikao kazi cha siku nne cha majaribio ya Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia Malalamiko na Rufaa kieletroniki Jijini Dodoma, Kamishina wa Sera ya Ununuzi wa Umma, Dkt. Frederick Mwakibinga amewasihi wadau wa ununuzi wa Umma kukipa uzito kikao kazi cha majaribio ya moduli hiyo ili kuwasaidia katika utendaji kazi wao.

“Leo tutakapopitishwa katika moduli hii, tuchukulie kama mafunzo lakini pia tutoe maoni yetu juu ya utendaji wa Moduli hii ili kuweza kufikia malengo yaliyotarajiwa na kuiwezesha PPAA kutoa haki kwa wakati na kujenga taswira nzuri ya Serikali,” alisema Dkt. Mwakibinga

Naye Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando amesema kikao kazi cha kufanya tathmini ya Moduli ya kuwasilisha malalamiko ni matokeo ya ushirikiano kati ya Mamlaka ya Rufani za Zabuni za Umma (PPAA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) katika kuhakikisha kuwa kigezo cha kupima mfumo kama uko sawa na unaweza kutumiwa na wadau wa ununuzi pamoja na taasisi nunuzi.

“Moduli hii inaokoa muda, na kutoa taarifa kwa PPAA kwa haraka kuliko ilivyokuwa awali. Aidha, Bw. Sando amesema kuwa kutokana na mabadiloko ya tehama ambapo imegusa kila nyanja hivyo kupitia tehama PPAA ikajenga Moduli hiyo ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kuliko hapo awali,” alisema Bw. Sando.

Mwaka 2004, Serikali iliifuta Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 3 ya Mwaka 2001 kutokana na upungufu uliokuwepo katika Sheria hiyo na kutunga Sheria Na. 21 ya mwaka 2004 ambayo ilitumika hadi mwaka 2011. Aidha, Serikali iliifuta Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya Mwaka 2011 na kutunga Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.10 ya Mwaka 2023 ili kukidhi mahitaji ya sasa ambayo yalishindwa kutekelezwa na Sheria ile ya 2011.

About the author

mzalendo