OR-TAMISEMI
Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba amesema takribani sh. Trilioni 11.5 zimetumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kuunufaisha na kuufungua kiuchumi Mkoa wa Kigoma ndani ya miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Katimba ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko mkoani Kigoma.
Amefafanua kuwa katika sehemu ya fedha hizo zaidi ya sh.Trilioni moja
zinatumika katika ujenzi na upatikanaji wa Nishati ya umeme kutoka Gridi ya Taifa ambao haujawahi kupatikana katika mkoa huo ambao upo Magharibi ya Tanzania ukipakana na nchi jirani za Kongo na Burundi.
“Na Leo Naibu Waziri Mkuu umeweka mawe ya msingi katika miradi mitatu ya
umeme katika mkoa wa Kigoma mradi wa uzalishaji wa umeme kutoka katika mto
Malagarasi, mradi wa njia ya kusafirisha umeme na kituo cha kupokea,kupoza na
kusambaza umeme, uwekezaji huu ni mkubwa na ukijumlisha fedha zote za
uwekezaji katika sekta ya nishati ya umeme katika Mkoa wa Kigoma zimekuja
shilingi Trilioni moja na zaidi,” amesema
Akizungumzia miradi ya umeme itakavyonufaisha sekta zilizo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Katimba amesema miradi ya umeme inayotekelezwa katika mkoa
wa huo itakwenda kunufaisha shule za msingi na Sekondari 983 na maeneo ya kutolea huduma za Afya ya msingi 324 ambayo yamewezeshwa vifaa na vifaa tiba
vinayotumia TEHAMA.
“Sisi Ofisi ya Rais – TAMISEMI ni Wizara inayoshughulika kwa kiasi kikubwa kutoa
huduma kwa wananchi mathalani katika sekta ya Elimu mkoa wa Kigoma kuna jumla ya shule za msingi na sekondari 983 shule zote hizi zinahitaji Nishati ya umeme kwasababu Mhe. Rais anafanya uwekezaji mkubwa na kuhakikisha kunakuwa na
maabara za TEHAMA lakini kwenye sekta ya Afya mkoa wa Kigoma una jumla ya
vituo 324 vya kutolea huduma ya Afya na vituo vyote hivi vinahitaji Nishati ya
Umeme,” amesema.