Featured Kitaifa

KAMATI ZA MAAFA WILAYA ZATAKIWA KUWEKA MIPANGO YA DHARULA

Written by mzalendo

Na Mwandishi wetu-SIMIYU

Serikali imezitaka Kamati za Usimamizi wa Maafa Ngazi ya Wilaya kuhakikisha zinajiandaa kikamilifu na kuweka mpango wa dharula wa utendaji na uratibu wa mawasiliano katika kukabiliana na maafa kwenye maeneo yao.

Maagizo hayo yametolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga, wakati akifungua mafunzo kwa Kamati ya Maafa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya maafa kwa kushirikiana na Shirika la World Vision Tanzania.

Aidha, Mhe. Nderiananga amezitaka taasisi zinazohusika na masuala ya usafiri, nishati pamoja na maji, kujiimarisha wakati wote ili kuhakikisha huduma za kijamii haziathiriki wakati wa maafa.

“Serikali ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga vyema kuhakikisha inakabiliana na maafa, tumeweza kununua vifaa vya kisasa kabisa ambavyo vinaweza kutupatia taarifa yoyote ya hali ya hewa inayotusaidia kujiandaa kabla ya maafa, wakati wa maafa na kurejesha hali,” alisema Naibu Waziri.

Sambamba na hilo Mhe. Nderiananga, ameipongeza Idara ya Menejimenti ya Maafa katika ofisi hiyo kwa namna inavyoshirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha inakabiliana na maafa pamoja na kurejesha hali katika baadhi ya mikoa iliyokumbwa na maafa ikiwemo mikoa ya Manyara- Hanang na Pwani.

Mbali na hayo, Naibu Waziri huyo amesema kuwa ikiwa kamati za usimamizi wa maafa pamoja na taasisi nyingine zinazohusika katika utoaji wa huduma za kijamii, zitaweza kuweka mikakati ya mapema gharama za kupambana na maafa zitakuwa kidogo na wananchi hawatakuwa na hofu.

Aidha, amebainisha kuwa serikali ya Rais Samia imefanya maboresho makubwa katika suala la utolewaji wa taarifa sahihi za utabiri wa hali ya hewa, ambapo kamati hizo zimetakiwa kutumia taarifa hizo katika kuweka mikakati hiyo.

Nae Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Oparesheni na Uratibu Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Luteni Kanali Selestine Masalamado alieleza kuwa, serikali kwa kushirikiana na Shirika la World Vision wanatoa mafunzo kwa kamati za maafa za wilaya ili kukabiliana na matukio hayo kwa ufanisi.

“Tunawashukuru sana World Vision kwani wao ndiyo wanafadhili mpango huu, katika mafunzo haya kamati hizi tunawaelezea namna sheria ya mifumo ya maafa ngazi ya Taifa hadi Kijiji inavyofanya kazi na majukumu ya kila kamati,” alisema Luteni Kanali Masalamando.

Vilevile Mkurugenzi wa Uetetezi, Imani na Maendeleo kutoka Shirika la World Vision Dkt. Joseph Mitinje alieleza kwamba shirika hilo limeshirikiana na serikali kutoa mafunzo hayo kwa kamati hizo ili kupunguza madhara yanayotokana na maafa.

Alisema, katika mpango wa mwaka huu, World Vision imepanga kutoa mafunzo kwa kamati za usimamizi wa maafa katika Wilaya 8 za Mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Tabora.

“ Tunatambua kuwa kamati hizi zikipewa elimu ya namna ya kuweka mipango ya mapema katika kupambana na maafa, kuelezwa majukumu yao katika kupambana na maafa, hatua hii itapunguza madhara yanayotokea kwa wananchi kutokana na maafa,” alisema Dkt. Mitinje.

Mwenyekiti Kamati ya Usimamizi wa Maafa Wilaya hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge, ameishukuru serikali pamoja na Shirika la World Vision Tanzania kwa mafunzo hayo, kwani yatawaongezea ujuzi, uwezo na maarifa katika kupambana na maafa kwenye Wilaya hiyo.

About the author

mzalendo