Featured Kitaifa

SERIKALI KWA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI YATOA MAFUNZO KWA WAJUMBE WA NACoNGO,WASAJILI WASAIDIZI MIKOA NA  HALMASHAURI 

Written by mzalendo

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu,akizungumza wakati akifungua  mafunzo ya siku mbili  kwa wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO) na Wasajili Wasaidizi kwa ngazi ya Mikoa na Halmashauri zote Tanzania bara yenye lengo la kuwajengea uwezo yaliyoanza leo Septemba 4,2024  jijini Dodoma.

Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao,,akizungumza wakati wa  mafunzo kwa wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO) na Wasajili Wasaidizi kwa ngazi ya Mikoa na Halmashauri zote Tanzania bara yenye lengo la kuwajengea uwezo yaliyoanza leo Septemba 4,2024  jijini Dodoma.

Wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO) na Wasajili Wasaidizi kwa ngazi ya Mikoa na Halmashauri zote Tanzania bara wakifatilia mafunzo  yenye lengo la kuwajengea uwezo yaliyoanza leo Septemba 4,2024  jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI kwa kushirikiana na sekta binafsi imefungua  mafunzo ya siku mbili kwa wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO) na Wasajili Wasaidizi kwa ngazi ya Mikoa na Halmashauri zote Tanzania bara yenye lengo la kuwajengea uwezo.
Akizungumza mara baada ya kufungua mafunzo hayo leo Septemba 4,2024 jijini Dodoma Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu,amesema matarajio ya mafunzo hayo ni kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Maafisa hao kuratibu NGOs.
Bi.Felister amesema Mashirika yataweza sasa kulipa ada kwa wakati, kuzingatia sheria,  kanuni na miongozo iliyowekwa katika kutekeleza majukumu yao.
Hata hivyo amesema kuwa  Wizara inatambua kuwa kuna changamoto mbalimbali katika uratibu kama vile, ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu sheria, kanuni na miongozo ya mashirika, mafunzo ya mfumo wa Kieletroniki wa usajili na uratibu (NIS), na ufinyu wa bajeti ya kufanya ufuatiliaji wa shughuli zao.
“Wizara inatarajia baada ya mafunzo hayo watahakikisha miradi inayotekelezwa na Mashirika inanufaisha jamii inayolengwa ili kuleta maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla.”amesema Felister.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Mwantumu Mahiza amesema kuwa  mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa wanaopatiwa wanafanya kazi kwa karibu na mashirika hayo  ambao ni wadau muhimu wa maendeleo.
“Nawataka Wasajili kufanya kazi kwa karibu na NGOs kwenye maeneo yao na kufuatilia shughuli wanazofanya kwa mustakabali wa nchi ya Tanzania.”amesema Mahiza
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Serikali (NaCONGO) Makala Jasper ameishukuru Wizara kwa ushirikiano inaotoa kwa mashirika yote nchini katika ngazi zote.
Awali Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao amesema kuna fursa nyingi za ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi kwa manufaa ya jamii hasa kupitia uanagenzi kwenye Vyuo vya Maendeleo ya Jamii.
Naye Mwakilishi wa Shirika la World Vision Tanzania Dkt. Joseph Mayala, amesema ni wakati muafaka wa ushirikiano kati ya Sekta binafsi na Serikali ns kuomba kiundwe Kikosi kazi ili kushiriki mjadala wa Sera ya Taifa ya Maendeleo unaoendelea pamoja na kuwa na mkakati endelevu wa mashirikiano.
Sambamba na mafunzo hayo, Wizara kwa kushirikiana na wadau, imezindua madawati ya uratibu wa NGOs kwenye sekta binafsi ili kuongeza ufanisi na kuimarusha ushirikiano.

About the author

mzalendo