Featured Kitaifa

TCU YAFUNGUA AWAMU YA PILI  UDAHILI WA  SHAHADA YA KWANZA MWAKA WA MASOMO 2024/2025

Written by mzalendo

 KATIBU  Mtendaji wa Tume ya Vyuo vikuu nchini (TCU) Prof. Charles Kihampa,akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 3,2024 jijini Dodoma wakati atangaza kukamilika kwa awamu ya kwanza na kufunguliwa kwa awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2024/2025.

Na.Meleka Kulwa-DODOMA

 

TUME ya Vyuo Vikuu nchini (TCU)  imefungua awamu ya pili ya udahili kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2024 – 2025 ambapo udahili utaanza leo septemba tatu hadi Septemba 21.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 3,2024 jijini Dodoma Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo vikuu nchini (TCU) Prof. Charles Kihampa,amesema kuwa  awamu hii itahusisha waombaji waliopata changamoto mbalimbali au kukosa nafasi katika awamu ya kwanza ya udahili.

“Tume inawaasa waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakuweza kupata nafasi ya kudahiliwa katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali,watumie fursa hiyo vizuri kwa kutuma maombi yao ya udahili kwenye vyuo wanavyovipenda”amesema Prof.Kihampa

TCU imeelekeza Vyuo vya Elimu ya Juu nchini kutangaza programu ambazo bado zina nafasi huku waombaji wa Udahili wa vyuo wanapaswa kuzingatia utaratibu wa awamu ya pili uliowekwa.

Aidha Prof.Kihampa amesema katika  kipindi cha mwaka wa masomo 2024 Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imedahili wanafunzi wa Shahada ya kwanza 198,986, ikilinganishwa na wanafunzi 186,289 katika mwaka wa masomo 2023 swa na na ongezeko la asilimia 6.8.

Pia, katika mwaka huu wa masomo programu zimeongezeka kutoka 809 kwa mwaka 2023/24 hadi 856 kwa mwaka 2024/25 ikiwa ni ongezeko la programu 47, huku akisisitiza kuwa hayo ni mafanikio makubwa kwa TCU.

Prof. Kihampa amesema kuwa  katika awamu ya kwanza ya udahili waombaji walikuwa 124,286 wakiwa wametuma maombi ya kujiunga na vyuo 86 vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi katika Shahada ya kwanza.

Amesema katika awamu ya kwanza ya udahili jumla ya waombaji 98,890 sawa na asilimia 79.6 ya waombaji wote walioomba udahili wamepata kwenye vyuo ambavyo wameomba.

Prof.Kihampa amesema kuwa idadi ya waombaji wa udahili inatarajia kuongezeka katika awamu ya pili ambayo imetangazwa kwa ajili ya wanafunzi weye sifa kuomba katika vyuo mbalimbali nchini.

Hata hivyo , amesema kuwa waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimoja ambacho anatarajia kwenda.

Amesema , uthibitosho huo, utafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliotumwa kwa ujumbe mfupi kwenye namba zao za simu au Barua pepe wakati wa kuomba udahili.

Prof.Kihampa amesema wale ambao hawajapata kwa wakati ujumbe huo wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalum ya siri ili kuweza kujithibitisha katika chuo husika.

“Waombaji wa Shahada ya kwanza wanakumbushwa kuwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katia chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika”amesema Prof.Kihampa

Hata hivyo, ametoa wito kwa wanafunzi kuchangamkia fursa za Udahili ambazo zimetolewa kwa awamu ya pili ili waweze
kupata nafasi za masomo ya kujiunga na vyuovya elimu ya juu.

About the author

mzalendo