Featured Kitaifa

ZANZIBAR YANUFAIKA NA FEDHA ZA MAZINGIRA

Written by mzalendo

 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali bungeni wakati wa Kikao cha 06 Mkutano wa 16 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 03 Septemba, 2024.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akishiriki Kikao cha 06 Mkutano wa 16 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 03 Septemba, 2024.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali bungeni wakati wa Kikao cha 06 Mkutano wa 16 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 03 Septemba, 2024.

……………..

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema jumla ya shilingi bilioni 5.3 zimepokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi Mhe. Bakar Hamad Bakar aliyetaka kujua kiasi gani cha fedha kimepatikana Zanzibar kwa miaka mitatu iliyopita kupitia Mifuko ya Kimataifa ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi. 

Mhe. Khamis amebainisha Serikali imekuwa ikipokea fedha kutoka kwenye Mifuko ya Kimataifa ya Mazingira na mabadiliko ya Tabianchi ikiwemo Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na Mfuko wa Mabadiliko ya tabianchi (GCF). 

Amefafanua kuwa fedha zinazotolewa zimekuwa zikitumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya hifadhi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi katika pande zote mbili za Muungano yaani Tanzania Bara na Zanzibar. 

Ametaja wilaya zilizonufaika kwa upande wa Zanzibar kuwa ni Wete na Micheweni (Pemba) kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula kwenye maeneo Mame nchini shilingi bilioni 1.2.

Halikadhalika, ametaja wilaya zingine kuwa ni Kaskazini A na Kaskazini B (Unguja) ambazo zimenufaika kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijijini – EBBAR shilingi bilioni 1.4 na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa wakazi wa Pwani shilingi bilioni 2.7.

Akijibu maswali ya nyongeza ya mbunge huyo kuhusu mikakati gani ya kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha Tanzania Bara na Zanzibar, Mhe. Khamis amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa maandiko 13 kwa ajili ya kuomba fedha zitakazosaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

”Ofisi ya Makamu wa Rais tumeshakaa na Sekretarieti za Mifuko inayohusika na utoaji wa fedha za uhifadhi wa mazingira kama nilivyoitaja hapo mwanzoni na tunapokaa nao tunawaeleza nchi zilizoendelea zitoe fedha kwa nchi zinazendelea.

”Pia kule Arusha kuna kikao kinaendelea cha Kamati ya Fedha ambacho kilifunguliwa jana (Septemba 02, 2024) na Mhe. Makamu wa Rais, yote haya tunafanya ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” ameeleza Naibu Waziri Khamis.

About the author

mzalendo