Featured Kitaifa

ZAIDI YA WASHIRIKI 2000 KUSHIRIKI JUKWAA LA MWAKA LA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI DODOMA

Written by mzalendo
 NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe.Mwanaidi Ali Khamis,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Septemba 2,2024 kuelekea Jukwaa la Mashiriki yasiyokuwa ya Kiserikali litakalofanyika kuanzia Septemba 4 hadi 6 mwaka  2024 jijini Dodoma.
MSAJILI wa Mashiriki yasiyokuwa ya Kiserikali Bi.Vickness Mayao,akijibu maswali yaliyoulizwa  na waandishi wa habari (hawapo pichani)  kuelekea Jukwaa la Mashiriki yasiyokuwa ya Kiserikali litakalofanyika kuanzia Septemba 4 hadi 6 mwaka  2024 jijini Dodoma.
MENEJA  Uchechemuzi na Jinsia kutoka Shirika la Word Vision Bi.Ester Mongi,akielezea jinsi walivyojipanga  kuelekea Jukwaa la Mashiriki yasiyokuwa ya Kiserikali litakalofanyika kuanzia Septemba 4 hadi 6 mwaka  2024 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA 
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Doto Mashaka Biteko  anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Jukwaa la Mwaka la Mashirika yasiyo ya Kiserikali ambapo zaidi ya washiriki elfu mbili kutoka nchi nzima watakutana kujadili namna ya  kuboresha huduma zao kwa jamii pia kutakuwa na huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kugharamia huduma hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 2,2024  na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Mhe.Mwanaidi Ali Khamis,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Jukwaa la Mashiriki yasiyokuwa ya Kiserikali litakalofanyika kuanzia Septemba 4 hadi 6 mwaka  2024 jijini Dodoma.
Mhe Mwanaidi amesema kuwa   Jukwaa hilo  la kitaifa limetanguliwa na Majukwaa ya Mashirika Yasiyo  ya Kiserikali katika ngazi za Wilaya na Mkoa ikiwa ni fursa ya mashirika yote kuweza kushiriki bila kuachwa nyuma.
“Lengo la majukwaa  ya Mashirika yasiyo ya kiserikali  katika ngazi za mkoa ni kubadilishana uzoefu fursa na changamoto katika utekelezaji washughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, mafunzo ya kujengeana  uwezo, utambuzi wa Mashirika yaliyofanya vizuri  na maazimio ya kushughulikia changamoto zilizoibuliwa na wadau mbalimbali.”amesema Mhe Mwanaidi
Aidha,Mhe Mwanaidi ameeleza kuwa Katika ngazi ya kitaifa siku ya kwanza yatafanyika  mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi na Wajumbe wa NaCoNGO wa Mikoa,Uzinduzi wa Madawati ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Sekta Binafsi na Majadiliano ya Pamoja na Wadau wa Sekta Binafsi.
“Vilevile, kutakuwa na mafunzo kuhusu Usimamizi wa Miradi, Uandishi wa Maandiko Dhana ya Miradi, Uandishi wa Taarifa ya Mfadhili na Ufuatiliaji & Tathmini; Programu za Huduma za Kijamii kupitia Dhana ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) katika eneo la Nkuhungu, Chamwino na Chang’ombe” amesema  Mhe Mwanaidi 
Hata hivyo  ameongezea kuwa siku ya pili kutakua na mijadala juu ya Fursa za Ndani na Nje ya Nchi za Ufadhili kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali; Mfumo wa Kisera na Kisheria wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali; Uzingatiaji wa Misingi ya Uwazi, Uwajibikaji, Uadilifu na Utawala Bora Katika Utendaji Kazi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
 Mhe Mwanaidi   amesema siku ya tatu itakuwa kilele cha Jukwa la Mwaka huu, ambapo baadhi ya shughuli zitakazofanyika siku hiyo ni pamoja na  Uzinduzi wa Kampeni ya Kutokomeza Njaa na Utapia mlo kwa Watoto, ambao utatanguliwa na matamko ya Wizara za Kisekta kuhusu Kutokomeza Utapiamlo kwa Watoto.
Aidha ametoa wito kwa wawakilishi wa wizara, idara na taasisi za kisekta, wajumbe wa bodi ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali, wasajili wasaidizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, Wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali, wawakilishi wa sekta binafsi, washirika wa maendeleo, vyombo vya habari, mashirika yasiyo ya kiserikali, wanufaika wa miradi na afua zinazotekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, wananchi wa mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani, pamoja na jamii kwa ujumla, kushiriki katika jukwaa hilo kwa mustakabali wa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali.

Kwa upande wake Msajili wa Mashiriki yasiyokuwa ya Kiserikali Bi.Vickness Mayao,amesema kuwa zaidi ya Mashirika elfu mbili yatashirika katika Jukwaa hilo.

Naye Meneja Uchechemuzi na Jinsia kutoka Shirika la Word Vision Ester Mongi amesema kampeni hiyo kwa kushirikiana na maendeleo ya jamii inategemea kufanyika katika mikoa yote ya Tanzania ikiaziwa mikoa 16 ambapo World Vision inapatikana.

Amesema wanatumia fursa hiyo ili waweze kupata wadau wengi katika kufikia mikoa mengine ambayo World Vision haipo.

“Tunashirikiana na Wizara 5 tukiamini kabisa wadau wote waliopo katika mikoa ambayo sisi hatupo wataenda kufanya ambacho sisi tunakifanya, lakini kampeni hii itadumu kwa miaka mitatu ilizinduliwa sasahivi hivyo ndani ya shirika tunategemea tuwe na bajeti isiyopungua dola milioni 3 katika kutekeleza kampeni hii,”

 “ Wadau tunaowategemea ni wote watakao kuwepo ukumbini na tuna amini wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali l, taasisi binafsi watafanya kitu katika nyazifa zao ili kutokomeza utapiamlo Tanzania.”

About the author

mzalendo