Featured Michezo

WAKALA WA VIPIMO YAPANGA KUNG’ARA SHIMUTA

Written by mzalendoeditor

Watumishi wa Wakala wa Vipimo wakifanya mazoezi ya viungo kabla ya kushiriki katika michezo mbalimbali

……

Ikiwa imebaki miezi miwili kuelekea mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma,Taasisi na Makampuni Binafsi ( SHIMUTA) ambayo yamepangwa kufanyika katika Viwanja vya CCM Mkwakwani mkoani Tanga kuanzia tarehe 10 hadi 24 Novemba,2024, Wakala wa Vipimo (WMA)imefanya bonanza la michezo leo Agosti 31,2024, katika viwanja vya Tcc Chang’ombe (Gwambina) Jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mashindano hayo.

Katika kuhakikisha kuwa WMA inapata timu bora na yenye ushindani, Watumishi wa Taasisi hiyo wameshriki michezo katika bonanza hilo ikiwemo mpira wa miguu,mpira wa pete, drafti, na kuvuta kamba ili kujiweka tayari na kuwa na utimamu wa mwili kuelekea SHIMUTA.

Akizungumza wakati wa bonanza hilo, Kaimu Mkurugenzi Huduma za Biashara wa WMA Bw. Karim Mkorehe ameeleza kuwa mazoezi ya kutafuta wachezaji wa kushiriki katika michuano ya SHIMUTA yameanza mapema ili kuhakikisha ushiriki wa taasisi unakuwa na tija.

Aidha, Mkorehe amesisitiza kuwa ufanyaji wa mazoezi ya pamoja huimarisha afya, na huleta umoja na hivyo kuwataka watumishi kujenga tabia ya kufanya mazoezi na kujenga utimamu wa mwili.

“Michezo ni afya na katika siku hii maalumu ya bonanza licha ya kucheza michezo mbalimbali pia watumishi wamepata nafasi ya kupima afya zao, pia wamepata chanjo ya homa ya ini na upimaji wa VVU ” amesema Mkorehe.

“Leo ni siku ya kwanza ya mazoezi yetu, tutakaa na kuandaa mpango mzuri wa mazoezi ya mara, tunatarajia kuongeza michezo mingine kama vile kukimbia mbio ndefu na fupi, lengo letu ni tuwe tayari kwa mashindano ya SHIMUTA na tufanye vizuri” ameongeza Bw.Mkorehe.

Kwa upande wake Mwandishi Mwendesha Ofisi wa WMA Bi. Hamida Salum ameupongeza Uongozi wa WMA kwa kuona umuhimu wa mazoezi kwa watumishi wake na kutoa wito kwa watumishi wote wa WMA kujitokeza kwa wingi na kushiriki mazoezi kwa mujibu wa ratiba husika.

“Leo tumejumuika watumishi wa WMA kutoka ofisi za makao makuu, Ilala,Temeke,Kinondoni na wenzetu wa mkoani Pwani katika bonanza hili, tumecheza tumefurahi na kuweka miili sawa, tukiwa na nia na kufanya vizuri mazoezini tutaiwakilisha vyema WMA katika SHIMUTA ya mwaka huu hapo Tanga” ameongeza Bi Hamida.

Mashindano haya ya SHIMUTA yalianzishwa mnamo mwaka 1967 na kusajiliwa rasmi mwaka 1973. Mashindano hayo hufanyika kila mwaka na huandaliwa kwa awamu na mikoa tofauti ambayo hupewa dhamana ya kuandaa mashindano kutoka kwa waratibu SHIMUTA. WMA itashiriki mashindano hayo kikamilifu.

Vikosi vya mpira wa miguu kutoka Wakala wa Vipimo vikiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mchezo

Timu za mpira wa pete za Wakala wa Vipimo zikiwa katika mazoezi wakati wa Bonanza la Vipimo katika viwanja vya TCC Chang’ombe

Timu ya Wanawake ya kuvuta kamba ikiwa katika mazoezi ili kujihimarisha kwa ajili ya kushiriki katika mashindano ya SHIMUTA

Watumishi wa Wakala wa Vipimo wakifanya mazoezi ya viungo kabla ya kushiriki katika michezo mbalimbali

Timu ya mchezo wa drafti ikijifua kwa ajili ya kushiriki mashindano mbalimbali

About the author

mzalendoeditor