Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), amesema kuwa ujenzi wa jengo jipya la ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Zanzibar lazima ukamilike kwa wakati bila kuathiri ubora.
Waziri Silaa alieleza hayo leo Agosti 19, 2024 wakati alipotembelea ofisi zilizopo Zanzibar na mradi wa ujenzi wa jengo jipya.
“Kwa kuwa mradi huu unatekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan, mafanikio yake yatakuwa ni mafanikio makubwa kwa Rais. Katika taarifa zenu, sijaona eneo lolote ambapo Serikali imekwamisha mradi. Hivyo, sisi watendaji tuliokabidhiwa majukumu haya, tunawajibika kusimamia mradi kwa ubunifu ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na ubora, bila kuvunja mikataba iliyosainiwa,” alisema Waziri Silaa.
“Tunataka baada ya muda uliopangwa, tukija hapa tuone kwamba jengo la ofisi ya TCRA Zanzibar limemalizika na wananchi wameanza kupata huduma.”
Waziri Silaa pia alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari, kuongeza juhudi ili ujenzi wa jengo hilo uweze kukidhi matarajio.