Featured Kitaifa

PROF.MKENDA:”MIFUMO YA ELIMU NCHINI LAZIMA IBADILIKE KUENDANA NA KASI YA MABADILIKO DUNIANI”

Written by mzalendo


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi, mifumo ya Elimu Nchini lazima ibadilike ili kufikia malengo kwa kuwapatia vijana ujuzi, maarifa na maadili kuwawezesha kustawi na kuhimili ushindani katika karne ya 21.

Mkenda amesema hayo leo Agosti 15, 2024 wakati akifungua Mkutano wa Elimu wa Kikanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Sherehe za Mwaka wa Elimu wa Umoja wa Afrika 2024 uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano WA Kimataifa wa Arusha (AICC).

Amesisitiza kuwa ni lazima tuhakikishe kuwa Elimu inayotolewa haihusu mafanikio ya Kitaaluma pekee, bali kuhakikisha inawezesha kwenda sambamba na mabadiliko ya Teknolojia pamoja na mabadiliko ya tabianchi.

“Tunasisitiza umuhimu wa teknolojia, mageuzi ya sera na ushirikiano ili kubadilisha mifumo ya elimu yenye kuwaandaa vyema vijana kwa ajili ya siku zijazo” Alisema Prof. Mkenda.

Waziri Mkenda ameipongeza kamati ya maandalizi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika ( AU), Mpango wa Elimu wa Kikanda Afrika, Chama cha Maendeleo ya Elimu barani Afrika (ADEA), Mtandao wa Hatua za Watu Kujifunza na wadau wote waliofanikisha Mkutano huo.





About the author

mzalendo