Featured Kitaifa

TCB YAJA NA SULUHISHO LA VIRUTUBISHO VYA ZAO LA PAMBA KWENYE MIMEA

Written by mzalendo

Afisa kilimo bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Mratibu wa Mbolea Hai Bw.Daniel Bariyanka,akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Kitaifa Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzunguni jijini Dodoma.

 Afisa kilimo Bodi ya Pamba Tanzania Renatus Filbert,akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Kitaifa Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzunguni jijini Dodoma.

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Afisa kilimo bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Mratibu wa mbolea hai Daniel Bariyanka amesema kwasasa bodi ya Pamba nchini imekuja na suluhisho la virutubisho vya zao hilo kwenye mimea yake ambapo wametengeneza mbolea hai ambayo inaweza kuwasaidia wakulima kwaajili kuweza kurutubisha mimea yao shambani.

Bariyanka ameyasema hayo leo Agosti 6,2024 Jijini Dodoma katika viwanja vya Nzunguni Nanenane wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na elimu wanayoendelea kuitoa kwa wakulima juu ya shughuli zao zinazoendelea katika banda lao.

“Mbolea hii ni mbolea ya maji yenye virutubisho vyote vikuu vitatu lakini pia yenye virutubisho vidogo vidogo vya aina tano, na tunaposema virutubisho vidogo vidogo na virutubisho vikubwa tunamaanisha kwamba mmea wowote ule hasa mmea wa pamba ili ukue na uzae vizuri unahitaji kupata virutubisho vya aina 17 ambapo kati ya hivyo ndipo vinakuwa virutubisho hivyo vidogo na vikubwa”, amesema.

Ameongeza kuwa mbolea hai hiyo waliokuja nayo ni ile ambayo wanaweza kuitengeneza katika mazingira au kwa kutumia malighafi yanayopatikana kwa wakulima wenyewe ikiwemo ile ya kutengeneza kwa kutumia kinyesi cha ng’ombe kibichi, majivu, mkaa, chokaa pamoja na kuongeza sukari.

“Tuna mbolea hai ambayo mkulima anahitaji kuichanganya sasa kwenye maji ili aweze kuipulizia kwenye mimea yake, mbolea hii tunamshauri mkulima baada ya kumaliza kupanda na pamba yake imeshaota siku 21 baada ya kuwa amepanda anahitaji kunyunyizia hii kwenye shamb lake kila baada ya siku 21 kwa mpulizo mmoja mmoja na mkulima anachanganya kiasi cha lita 2 kwa pampu moja,”ameongeza.

Pia ametoa wito kwa wakulima baada ya kupata elimu hiyo na mbolea waitumie sana mashambani, kwasababu ndiyo suluhisho la virutubisho ambavyo vinapatikana katika mimea ya pamba ili mmea wa pamba uweze kukuwa vizuri.

Naye Afisa kilimo Bodi ya Pamba Tanzania Renatus Filbert ametoa wito kwa wakulima kufuata kanuni za kilimo bora cha zao hilo hasa kuzingatia kipimo kipya cha upandaji cha sentimita 60 mstari kwa mstari na sentimita 30 mche kwa mche.

“Kipimo hiki kimeonesha ufanisi kwa kuongeza uzalishaji wa eneo ambapo zaidi ya 70% sasa ya wakulima wameweza kwasasa kufuata hiki kipimo na matokeo yake sasa imeonekana kwanza wakulim wengi wameanza kupata mavuno mengi ya kuanzia kilo 1000 kwa hekari, kwahiyo tunahamasisha sana wakulima wetu kufuata hiki kipimo kwa kufuata kanuni zile nyingine za kilimo bora cha pamba”, amesema.

About the author

mzalendo