Featured Kitaifa

RAIS SAMIA AMEWAJALI WANYONGE KWA KUWAPA MSAADA WA KISHERIA

Written by mzalendo
Maofisa wa Msaada wa Kisheria wakisikiliza wananchi waliofika kwenye banda la maonesho la Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika viwanja vya nanenane Nzuguni jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imepiga kambi katika maonesho ya nanenane viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma huku wananchi wakimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa msaada huo huku wakishauri iwe taasisi ya kudumu itakayowasaidia kupata haki zao kwenye migogoro ya kisheria.
Msaada huo unalenga kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu ya sheria, huduma za ushauri, na ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya kisheria wanayokumbana nayo katika maisha yao ya kila siku.
Katika Maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kukutana na wataalamu wa sheria ambao wanaweza kuwasaidia kuelewa na kutatua matatizo yao.
Mkazi wa Kigamboni, Lameck Kipiliango amesema “Nimefurahi sana kuwepo kwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi napendekeza kama itampendeza Rais Samia hii isiwe tu kampeni maana kampeni inaisha muda ila ikiwa Taasisi ya kudumu itawasaidia sana wananchi wanyonge ambao wanapambana sana kusaka haki zao kisheria.”
Kipiliango amesema amefika katika banda hilo ili kusaidiwa kupata ufumbuzi wa mgogoro wake wa ardhi na Jiji la Dodoma.
“Nimefurahi nimepata msaada wa kisheria unaohusiana na mambo ya ardhi nimeona kama ni Mungu aliniongoza nije hapa nimefurahi sana, tunamshukuru sana mama ameleta kitu kipya huko nyuma hakikuwepo,”amesema.
Amesema wananchi wanapendekeza iwe taasisi ya kudumu na endelevu kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kama ilivyo Taasisi ya Benjamin Mkapa.
Mwananchi Esther Lihofo amesema “Nimetembelea banda hili la sheria la Mama Samia nimekutana na Ofisa anaitwa Koku amenipa ushauri na elimu nzuri kuhusu masuala ya kisheria najipanga vizuri kwenye kuweka mirathi.”
Amesema mpango huo ni mzuri katika kuwasaidia wananchi wasio na uwezo ambao hawana uwezo wa kuweka Mawakili.
“Hapa kwa msaada wa mama tunapata msaada wa kisheria bure tunamshukuru Rais Samia kweli ni Rais wa wanyonge,”amesema.
Mkazi wa Area C Dodoma, Thomas, amesema katika maonesho ya nanenane amejifunza kupitia kampeni hiyo itasaidia wananchi wengi wasiokuwa na uelewa wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kampeni hii ambayo imepiga kambi hapa nanenane Dodoma itawasaidia wananchi na watanzania kwa ujumla,”amesema.
Naye, Mkazi wa Hombolo, Lenard Hamis amesema amepata huduma nzuri kwenye banda la kampeni hiyo na amejifunza mambo ya kisheria ya kufuata na kutoa elimu kwa wananchi wenzao wa vijijini.
“Tumepewa namba za kupiga kwa ajili ya msaada wa kisheria tutawapa watendaji wasambaze kwa wananchi ili wanufaike na huduma hii ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, tunamshukuru sana Rais hakika mama anaupiga mwingi kwa wananchi wake,”amesema.
Mkazi wa Jiji la Dodoma, Yusuph Masatu, amesema amefarijika kupata huduma nzuri ambayo hakutegemea kuipa ya elimu ya masuala ya sheria.
“Nimshukuru Rais kwa kuona umuhimu wa kampeni hii, kweli watu ni wanyonge hawawezi kupata msaada wa kisheria kuwa na mawakili lakini ameliona hilo na kuleta kampeni hii ambayo itawasaidia sana watanzania tunashukuru sana,”amesema.

Maofisa wa Msaada wa Kisheria wakisikiliza wananchi waliofika kwenye banda la maonesho la Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika viwanja vya nanenane Nzuguni jijini Dodoma.

About the author

mzalendo