Featured Kitaifa

TLS INAHITAJI RAIS SI MWANAHARAKATI

Written by mzalendoeditor

 

Na Mwandishi wetu

Ikiwa imesalia siku moja kufanyika uchaguzi wa nafasi mbalimbali ndani ya Chama cha Mawakili Tanzania (TLS) ikiwamo Urais, Mawakili wabobezi Julius Mtatiro na Ally Kileo wametoa uchambuzi wao kuhusu wagombea sita waliopo kwenye kinyang’anyiro cha Urais huku wakionesha Sweetbert Nkuba na Boniface Mwabukusi wana nguvu ya ushawishi wa kuwa Rais wa TLS.

Katika nafasi hiyo, wagombea wengine wanaowania ni Capt. Ibrahim Bendera, Emmanuel Muda, Revocatus Kuuli na paul Kaunda.

Katika andiko lao, Mawakili hao wamewachambua wagombea kupitia mijadala mbalimbali waliyoshiriki ikiwamo mjadala wa wazi uliorushwa na Star TV.

Wanasema wametoa uchambuzi wao ili kuongeza na kushajiisha mjadala unaoweza kusababisha TLS ikaendelea kupata viongozi bora watakaoendeleza kazi nzuri kwa mujibu wa sheria inayounda Chama hicho wameona watoe uchambuzi huo kwa wagombea ambao wanadhani wanaweza kuweka ushindani wa kipekee katika kinyang’anyiro cha urais wa TLS.

“Hii ni kwa sababu, licha ya kuwa tunatambua umuhimu wa wagombea wote, lakini tunatumia uhuru wetu wa kichambuzi kunoa shabaha ya mielekeo halisi ya nani na nani wanaonekana wana nguvu dhahiri katika kinyang’anyiro hiki na wana nafasi ya kukwea katika nafasi ya juu kuliko wengine,”wanasema

Wanaongeza kuwa “Wengi wetu tumejifunza kuwa wagombea wote sita waliofuzu ni wazoefu na wana sifa mbalimbali za kiuongozi. Kila mmoja ana sifa za kipekee tofauti na wenzake na kila mmoja akiwa na uzoefu wa kipekee ambao si lazima ufanane na mwingine, na kwa hiyo ni wazi kuwa kila mgombea anaweza kuleta mabadiliko fulani au matatizo fulani atakavyopata nafasi ya kuhudumu urais wa TLS.”

Wanasema kabla hawajafanya uchambuzi huo walijiuliza maswali mbalimbali kama msingi wa kile kinachoweza kutokea TLS na mwelekeo wake kwa siku zijazo.

Wanasema ni wazi kwamba, TLS kwa sasa kinahitaji Rais ambaye haji kujianzishia tu mambo yake vile atakavyo.

Pia, TLS kinahitaji Rais ambaye atakuja kuendeleza na kuweka mkazo kwenye mambo muhimu na mazuri (misingi) iliyowekwa na watangulizi wake, yaani Mawakili Profesa Edward Hosea na Harold Sungusia ambao wamefanya majukumu yao hivi karibuni – pamoja na kurekebisha maeneo ambayo hayakufanyika vizuri, bila kusahau kujenga uwezo wa kuwaunganisha mawakili.

SIFA ZINAZOTAKIWA

Wanasema TLS ni Chama cha kitaaluma kinahitaji Rais mtendaji, mweledi, mtulivu, mwenye uwezo wa kushawishi wadau wote wa sheria ndani ya nchi, mwenye maono yanayoweza kutekelezeka bila papara. Atakayeweza kuwaunganisha mawakili wote, atakayekua kiungo muhimu kati ya TLS na mdau mkuu ambaye ni Serikali, na ambaye hatogeuka kuwa “msanii na mpiga kelele”, kueneza chuki kwa misingi ya uanaharakati, utofauti wa ufuasi wa vyama vya siasa, mihemko na jazba.

Wanasema TLS inahitaji mtu mwenye visheni na busara za kutosha, ambaye anaweza kukisaidia Chama cha Mawakili kutekeleza majukumu yake katika hali ya utulivu na ufanyaji maamuzi wa pamoja na wenye tija.

NKUBA VS MWABUKUSI

Wanasema wamechambua mawakili wote wanaogombea nafasi ya kiti cha urais wa TLS, ni nani miongoni mwao wanaoonekana wana ushawishi, kwa nini? Baada ya ufuatiliaji na uchambuzi wa kina, kati ya wagombea wote waliojitokeza kwenye nafasi ya kiti cha urais TLS, Mawakili Mwabukusi na Nkuba wanaonekana kuwaa na ushawishi zaidi miongoni mwa wapiga kura mawakili.

MWABUKUSI ana ushawishi?

Wanasema Wakili huyo hivi karibuni amekuwa akijijengea umaarufu kwa sababu ya misimamo yake mikali dhidi ya serikali, mamlaka mbalimbali za nchi pamoja na kupinga mara kwa mara mwenendo wa mahakama ya Tanzania.

Kwa sababu hiyo, lipo kundi la vijana ndani na nje ya tasnia ya sheria linaloamini kuwa TLS inahitaji mtu atakeyeendesha mapambano ya kutosha dhidi ya serikali na mahakama kwani Mwabukusi anao uwezo wa kutamka lolote, muda wowote na bila kujali chochote.

Anajiamini kupita kiasi na ana uwezo wa kufanya lolote bila kujali mamlaka zilizopo.

Wakili Mwabukusi ameweka wazi kuwa atakapokuwa Rais wa TLS atashawishi na kulazimisha mabadiliko katika sera, hali, na sheria mbalimbali hata kama ni kwa kutumia nguvu ya maandamano n,k. Wakili Mwabukusi amekua mara nyingi akisisitiza kwamba haki haiombwi bali hudaiwa ikiwezekana hata kwa kutumia nguvu.

“Misimamo hii ni miongoni mwa sababu zinazomfanya apate ufuasi ndani na nje ya tasnia ya sheria hususani kutoka makundi ya vijana. Mwabukusi na kampeni zake kupitia vyombo kadhaa vya Habari ikiwemo na mitandao ya kijamii, anapata ufuasi kwa sababu amejipambanua kwa dhati kama mtu anayeamini kuwa uhusiano na ufanyaji kazi wa TLS na serikali na mahakama, ni janga lisilokubalika,”wanasema.

Wanafafanua kuwa huo ni mtego ambao unaweza kuifanya TLS isifikie malengo ya mawakili na kwa hiyo anaamini kuwa TLS ya ndoto zake ni ile ambayo itakaa upande mmoja, kisha serikali ikae upande wake na mahakama ikae kwake kisha wadau hawa watatu waanze mapambano.

Wanasema Mwabukusi katika hotuba zake amekuwa akisisitiza na kuongea kwa jazba kuwa hajawahi kushindwa na hamwogopi mtu yeyote yule. Mwelekeo wa namna hii kwa kawaida na msingi wake ni mlipuko na mhemko ambao baadaye huleta majuto.

MISIMAMO YA MWABUKUSI HAINA TIJA

Wakizungumzia misimamo na mwelekeo wa Mwabukusi kama una tija yoyote ndani ya TLS, wanasema kwa uchunguzi na uchambuzi wa kina walioufanya, wanajiridhisha na kuamini kuwa misimamo na mwelekeo wa Wakili Mwabukusi hautokua na tija ya aina yoyote kwa kipindi chote cha miaka mitatu endapo atapata fursa ya kuwa Rais wa TLS.

“TLS ni chombo cha kisheria na kinajiendesha kwa mujibu wa sheria na vikao. Mwelekeo huu wa Wakili Mwabukusi unamaanisha kuwa TLS itageuzwa kuwa uwanja wa mapambano ya siasa kali badala ya kuwa uwanja wa majadiliano, ushawishi, maridhiano, uunganishaji wa wadau (serikali na vyombo vyake kwa upande mmoja na mahakama kwa upande mwingine),”wanasema.

Hata hivyo, wanasema matamko na misimamo mikali ya wakili Mwabukusi ingeweza kuwa na tija kubwa endapo chama cha TLS kingelikuwa ni Chama kilichosajiliwa na msajili wa vyama vya siasa Tanzania kuwa na malengo makuu ya kushiriki siasa ndani ya nchi.

“TLS sio chama cha Siasa. TLS hakikusajiliwa kwa mujibu wa sheria ili kushindana kwenye ulingo wa siasa na vyama vingine vya siasa au kupambana na serikali au kujenga hoja za kimapambano ili kipate uungwaji mkono. TLS imeundwa kwa ajili ya kulinda na kusaidia wananchi kuhusiana na mambo ya kisheria kwa njia halali za kisheria. Lakini inao wajibu mkubwa na wa kwanza kuwakilisha, kulinda na kusaidia na kusimamia ustawi na maslahi ya wanachama wake.”

“Kwahiyo, mtu yeyote anayetaka kuiongoza TLS anapaswa atuletee maono yenye uthabiti na ushawishi wa kisheria na kimantiki, ili tuwe na uhakika kwamba huyu tukimpa nafasi hii, atasimamia maslahi na ustawi wa wanachama na kuwa muunganishaji na daraja zuri la mawakili kuifikia serikali na vyombo vyake, vilevile mahakama na ngazi zake. Kinyume na hapo, sarakasi za matamko ya mitaani, jazba, vurumai, hekaheka za kisiasa na matamko ya kisiasa, haviwezi kuwa sehemu ya TLS ile iliyoundwa kwa mujibu wa sheria na ambayo inajikuza ili kujenga mawanda ya utendaji kazi ya PALU na BLA,”wanasema

Kwa nini Wakili NKUBA ana ushawishi kuiongoza TLS 2024-2027?

Wachambuzi hao wanasema Wakili Nkuba katika matamko na mielekeo yake mbalimbali kwa TLS, amejipambanua wazi kuwa anakwenda kuwa Rais wa TLS, kwanza kuanzia pale walipoishia watangulizi wake mbalimbali, lakini akiweka mkazo kwenye eneo la kuimarisha mahusiano ya kimsimamo kati ya TLS na Mahakama na Serikali ili mahusiano hayo yawe chachu ya upenyezaji wa ushawishi na ajenda mbalimbali ambazo ni kilio cha mawakili, na hasa mawakili vijana.

Wanasema Wakili Nkuba anaamini serikali na mahakama ni wadau wasiokwepeka, na kwamba TLS haiwezi kamwe kufanya kazi peke yake kwa kujifungia na kazi hizo zikafanikiwa.

“ Wakili Nkuba anaamini kuwa TLS siyo jukwaa la kuendeleza malumbano na mapambano ya kisiasa, na badala yake ni jukwaa la kisheria linalojiendesha kwa vikao na mipango ya ndani iliyojaa utulivu na ushawishi wenye misimamo.”

“Katika hotuba zake Wakili Nkuba amejipambanua kama kiongozi aliyetulia, mwenye maono chanya na mwenye kiu na ndoto kwamba TLS inaweza kusonga mbele na kuwa sehemu ya mabadiliko muhimu ya kisera, kisheria, kikatiba n.k masuala ambayo yameonekana kuwa kipaumbele muhimu katika Serikali ya Awamu ya Sita,”anasema

Kwa sababu hizo, wanasema Nkuba amejenga ufuasi kutoka kwa wapiga kura wanaoamini kuwa TLS ili ishawishi mabadiliko mbalimbali yanayolinda hadhi na tasnia ya sheria na mawakili nchini Tanzania, inahitaji utulivu na shabaha halisi zitakazotekelezwa kimkakati na kwa dhana ya kutambua kuwa serikali na mahakama ni washirika muhimu katika michakato ya TLS.

MISIMAMO YA NKUBA INATIJA

Kadhalika, wakizungumza kuhusu misimamo na mwelekeo wa Nkuba una tija yoyote ndani ya TLS, wanasema wanaamini mwelekeo na msimamo wa Nkuba unaweza kuwa na tija ndani ya TLS.

“ Ukweli ni kwamba TLS siyo jukwaa la mapambano ya barabarani, siyo eneo la vita wala siyo eneo la kushughulikiana na watu, serikali au mahakama. TLS ni chombo kinachoheshimika sana, ni jukwaa la kisheria linalopaswa kukaliwa na watu wanaofikiri sawa sawa, kwa ujasiri na utulivu, watu wanaoamini kuwa ni lazima wafanye kazi na wadau wengine bila kutukanana na kupambana ili wafikie malengo ya pamoja ya nchi – kwa sababu malengo hayo siyo ya mtu mmoja au kundi moja.”

“Wakili Nkuba ni mfano halisi wa kiongozi kijana, mtulivu, mwenye maono na anayeamini katika misingi ya ndoto zilizofikiwa na PALU na BLA, ambazo TLS inaweza kuzifikia kirahisi ikijiwekea malengo.”

“Ni kijana kiongozi anayeamini kuwa uongozi ni ajenda za pamoja, uongozi ni ushirikishaji na ushirikishwaji, na uongozi ni vile ambavyo kiongozi anajiweka miongoni mwa wenzake ili kulinda maslahi yao na kuheshimu maslahi ya kisheria ya mamlaka zingine,”Wanasema.

NKUBA NI RAIS BORA TLS

Wanasema Tukiwa ni mawakili ambao ni sehemu ya TLS tuna uhakika asilimia mia moja kuwa, Nkuba atakuwa ni Rais bora zaidi wa TLS kuliko Mwabukusi.

“Sehemu ya uchambuzi huu imegusia kwa kina ni namna gani wawili hawa wana uwezo wa namna gani na wanaweza kuwa Marais wa namna gani. Ni wajibu wetu kuyasema haya kwasababu hiyo ni njia ya kufumbua macho ya kila mmoja wetu ili mwisho wa siku kila kura itakayopigwa iwe kura ya mfano, yenye kuleta TLS inayohitajika katika muktadha wa wakati wa sasa na TLS inayoweza kujifunza na kujitengeneza kuwa PALU na BLA siku zijazo,”Wanasema.

About the author

mzalendoeditor