Uncategorized

WAUGUZI BMH WADHAMIRIA KUFANYA KAZI KWA KUJITUMA PAMOJA ILI KUBORESHA HUDUMA ZA TIBA

Written by mzalendo

Na Jeremiah Mbwambo, Dodoma

Ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma, wauguzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wamekubaliana kufanya kazi kwa kujituma zaidi na kama timu wanapohudumia wagonjwa.

Wameyasema hayo leo wakati wakiongea na Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, katika kikao cha kufahamiana na kushirikishana mwelekeo wa Hospitali na dhana ya ubora wa huduma za tiba.

Muuguzi Ndg Moabu Thobias kutoka CCU ameshauri kuwe na ushirikiano kati ya wauguzi na madaktari wanapozungukia wagonjwa wodini, na kuheshimiana kila mmoja.

“Nashauri kuwe na teamwork (kufanya kazi kwa pamoja) kati ya madaktari na wauguzi wanapowazungukia wateja ili kuongeza ufanisi wa kutoa huduma,” amesema Ndg Thobias.

Ndg. Matuga Mwamtende, muuguzi kutoka Kliniki ya Damu, ameshauri BMH kuanzisha kliniki ya huduma mkoba kusaidia kutoa elimu kwa wananchi juu ya huduma inayotolewa na kliniki husika.

“Tuwe na clinic outreach (Huduma mkoba ya kliniki) ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa yanayotibiwa na kliniki husika,” amesema.

Wamesema madaktari wanapowazungukia wateja wodini, mbali ya madaktari kuambatana na wauguzi, lakini pia timu ya watoa huduma iambatane na wafamasia na wataalamu wa maabara.

“Naomba tuwe na round (kuzungukia wagonjwa) shirikishi wodini kwa kushirikiana na wafamasia, wataalamu wa maabara na madaktari,” amesema Sr Eveline Omire, Muuguzi Kiongozi kutoka ICU.

About the author

mzalendo