Featured Kitaifa

WAZIRI SIMBACHAWENE- SIASA ZA KISASA NI KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI NA SI KUPIGA MANENO MATUPU

Written by mzalendo

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene   akizungumza leo na wananchi wa Kata ya Kibakwe iliyopo katika Jimbo la Kibakwe,  Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Jijini Dodoma, ikiwa ni ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi  katika Jimbo hilo.

Sehemu ya wananchi wa Kata ya  Kibakwe iliyopo katika Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Jijini Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, wakati wa  ziara ya kikazi ya Waziri huyo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi  katika Jimbo la Kibakwe

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali pamoja na wananchi akikagua ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami  unaoendelea  katika eneo la kuelekea Shule ya Sekondari Kibakwe na Kanisa Katoliki  ikiwa ni ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi  katika Jimbo hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali pamoja na wananchi akikagua ujenzi wa Chuo cha VETA unaoendelea  katika Jimbo la Kibakwe  ikiwa ni ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi  katika Jimbo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. Sophia Kizigo  akizungumza na wananchi wa Kata ya Kibakwe iliyopo katika  Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya  Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene   kuzungumza na wananchi hao ikiwa ni  ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi  katika Jimbo la Kibakwe. 

………………. 

Na Mwandishi wetu – Kibakwe

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe.George Simbachawene amesema siasa za kisasa ni kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na sio kuzungumza maneno matupu huku akiwataka wananchi kuwapuuza wale wote wanaokejeli maendeleo yaliyofanywa na Serikali jimboni kwake na nchini kote kwa ujumla.

Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kibakwe iliyopo Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma ambapo amesema Kibakwe ya  sasa ni  tofauti sana na ile ya miaka kadhaa iliyopita, huku akitolea mfano kuwa mwaka 2005 jimbo hilo lilikuwa dhoofu sana kwenye huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji, umeme pamoja na barabara.

“Kibakwe ninayoiona leo inafurahisha sana, tumetekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo na kwa kiasi kikubwa sana kwani utitiri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa mnaiona wenyewe” amesema Mhe. Simbachawene.

Akizungumzia mradi wa miundombinu ya barabara jimboni humo, Mhe. Simbachawene amesema Kibakwe ya sasa imefunguka huku akitaja uwepo wa barabara za lami pamoja na utengenezaji wa barabara kila kona katika Jimbo hilo ukiwa unaendelea.

“Leo tumekagua ujenzi wa barabara ambapo mmeshuhudia wenyewe  uwekaji wa lami kuelekea Shule ya Sekondari Kibakwe pamoja  na  kuelekea Kanisa Katoliki ukiwa unaendelea, hizi ndizo siasa za kileo” amesisitiza Mhe. Simbachawene.

Ameongeza kuwa taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutokea  Mpwapwa hadi  Kibakwe unaendelea.  

Aidha, Mhe. Simbachawene amezungumzia mradi mwingine wa ujenzi wa Chuo cha VETA unaoendelea katika Jimbo hilo la Kibakwe utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.6 hadi kukamilika kwake ambapo amesema ukikamilika utatatua changamoto ya ajira kwa vijana nchini, hususan katika Jimbo hilo la Kibakwe.

Amefafanua kuwa, chuo hicho cha VETA mara baada ya kukamilika kwake kitasaidia kuwaandaa vijana kujiari badala ya kusubiri kuajiriwa huku akisema vijana watakaohitimu chuoni hapo watachochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, huku akisema katika Jimbo hilo kila Kata ina shule  zaidi ya moja ya  ya Msingi na  Sekondari.

Vile vle Mhe.Simbachawene ameongeza kuwa huduma za afya katika Jimbo la Kibakwe zimeboreshwa sana  tofauti na mwanzo  ambapo amesema Kituo cha Afya cha Kibakwe ambacho kwa sasa kina hadhi sawa na Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa kwani kina vifaa vya kisasa ikiwemo majokofu ya kuhifadhia miili,  vifaa vya huduma za  dharula  pamoja na huduma ya afya ya mama na mtoto.

Wakati huohuo, Mhe. Simbachawene ametambua jitihada za mtu mmoja mmoja zilizofanywa na wananchi wa Kibakwe na kuchangia maendeleo ikiwemo ujenzi wa  nyumba za kisasa katika jimbo hilo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kibakwe, Mhe. David Chisanza amemuelezea Mhe. Simbachawene kuwa ni Kiongozi wa mfano ambaye  katika kipindi chote cha uongozi ameendelea kuzigusa familia za wana Kibakwe kwa namna tofauti kimaendeleo.

About the author

mzalendo