Featured Kitaifa

KINANA AWASHAURI VIONGOZI CCM KUZINGATIA MAADILI

Written by mzalendo

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Mapinduzi (CCM) Abdulrahman akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la malezi na maadili lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania, mjini Mpanda, Mkoa wa Katavi. (Picha na Fahad Siraj-CCM)

Na Mwandishi Wetu

 
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Abdulrahman Kinana amewasisitiza wananchi na viongozi mbalimbali hususan wanaotokana na Chama hicho kuwa mfano bora wa maadili na malezi mema nchini.
 
Pia, amewakumbusha viongozi wa CCM kuwa waadilifu kwa kauli, vitendo na mwonekano na wasikubali kuwa sehemu ya Chama na viongozi wake kusemwa vibaya kwa kutozingatia maadili.
 
Akizungumza Leo mjini Mpanda, mkoani Katavi alipofungua Kongamano la Malezi na Maadili lililondaliwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama hicho, Kinana alisema kongamano hilo linazungumzia malezi na maadili mambo ambayo ni muhimu na hutegemeana.
 
“Yanaanza malezi halafu yanakuja maadili, mimi sio mwanafalsafa lakini katika vitu siamini kwamba kuna maadili mabaya, neno maadili ni neno nzuri tukiangalia vitabu vya dini vinaeleza kuwa maadili ni jambo jema.
 
“Jambo jema huwezi kuhusisha na jambo baya, kwa maoni yangu hakuna maadili mabaya. Nadhani kuna malezi mabaya, tabia mbaya, kuna mwenendo mbaya, lakini hakuna maadili mabaya. Maadili ni jambo jema na tunatakiwa tuwe na maadili mazuri,” alisema.
 
 Alifafanua kuwa, maadili yanapatikana kutokana na malezi na mafunzo na wanaofanya kazi hiyo ya kujenga malezi mema na maadili kwanza ni familia, ndio maana wanasema malezi. Pili ni jamii kwa ujumla wake ambayo nayo inadhamana ya kujenga maadili kupitia malezi.
 
“Tatu, wanapokwenda shuleni kuanzia elimu ya awali, msingi mpaka vyuo vikuu tunasimamia malezi na kujenga maadili. Malezi na mabadiliko vinajengwa pia na taasisi mbalimbali, maadili ni jambo muhimu katika maisha yetu ya binadamu, ndio maana vitu vingi havisisitizwi lakini jambo kubwa linalosisitizwa ni maadili.
 
“Hatusemi kuna maadili mabaya ila kuna mmomonyoko wa maadili, maana yake kiwango cha maadili kimeshuka kwa sababu madili ni jambo jema. Mtu mwenye maadili ni muungwana, mzuri, anayejiheshimu na kuheshimu wenzake. Mtu ambaye amejaa sifa ni mtu mwenye maadili,” alisema.
 
Alisema kuna umuhimu wa kila mwananchi kuwa mwadilifu katika maisha ya kila siku kwani ni jambo ambalo linasisitiwa hata katika vitabu vya Mwemyezi Mungu.
 
Alifafanua kuwa kazi ya CCM na serikali ni kusimamia maadili na kwa upande wa Chama kumekuwa na vikao katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya mata, wilaya, mkoa hadi taifa.
 
“Katika ngazi kuna kamati ya maadili. Ngazi  ya taifa, kamati ya maadili mkoani, wilayani, kata mpaka chini na hii inadhihirisha umuhimu wa maadili. Ili tuwe na jamii bora inayojithamini na kuheshimu lazima kuzingatia maadili bora, hata serikali inasimamia maadili.
 
“Unaposikiliza kaulimbiu mbalimbali zinazotolewa na viongozi ni tafsiri ya kutakiwa kuwa muaminifu. Kumekuwa na kauli za kukemea rushwa na Katiba ya CCM inasema sitatoa wala kupokea rushwa kwa sababu rushwa ni audui wa haki. Kutoa rushwa unavunja uadilifu,” alisema.
 
Pia, alisema kuna kamati ya taifa ya serikali inayosimamia maadili ya viongozi, hakuna kamati zingine zinazosimamia maendeleo au mambo mengine lakini kuna kamati ya kusimamia maadili.Yote hiyo ni kudhihirisha umuhimu wa maadili.
 
“Sisi viongozi tunatakiwa kuwa mfano wa maadili na hasa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kuepuka mambo yote ambayo yataleta sifa mbaya kwa Chama Cha Mapinduzi au kuleta sifa mbaya kwa wana CCM na viongozi wake.
 
“Tunawajibu wa kuyasimamia maaadili, maadili ni mambo yote mema na kueupka mabaya. Sisi viongozi ndani ya CCM tunatakiwa wakati wote kuwa mfano kwa kauli zetu na vitendo vyetu kwa maisha yetu yote.Tuwe mfano wa uadilifu, kila anayekuona uwe tafsri ya maadili, tuwe tafsiri ya sifa za uadilifu,” alisema.
 
Alisema kauli zinazotolewa na viongozi mbalimbali zinadhihirisha maadili, kukemea rushwa, mambo yasiyo mema kwa jamii na kuhimiza kujenga undungu, mshikamano na kusaidiana.
 
Aliongeza hata kaulimbiu za waasisi wa taifa wakiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ziliakisi umuhimu wa maadili.
 
“Hata leo tangu baba wa taifa afariki dunia miaka 28 iliyopita lakini kauli zake zimebakia hai kwa kuwa alikuwa mwadilifu. Ndio maana hadi leo tunaendelea kunukuu kauli zake katika masuala mbalimbali. Sio viongozi wengi wa Afrika ambao wanakumbukwa na kufanyiwa rejewa kama anavyofanyiwa Mwalimu Nyerere.
 
“Fuatilia viongozi wote walioleta uhuru katika Bara la Afrika ambao baada ya miaka 30 ya uhuru bado wanakumbukwa lakini Mwalimu Nyerere amebakia kuwa mfano bora na yuhai kwasababau ya uadilifu wake,” alisema.
 
Aliongeza viongozi wa CCM wanawajibu wa kuendelea kuwa waadilifu kwa kauli na vitendo huku akiipongeza Jumuiya ya Wazazi kwa kuandaa kongamano hilo kubwa kuzungumzia maadili na malezi.
 
“Mtakumbuka kabla ya kuitwa jumuiya ya wazazi huko nyuma ilikuwa inatwa TAPA, kwa maana ya ‘Tanzania Parents Association’ kwa sababu jumuiya ya wazazi ndio inayojenga malezi na maadili katika Chama.
 
“Kupitia kongamano hili itaangaliwa hali ya maadili ikoje, tufanye nini ili tuendelee kuwa na maadili katika nchi yetu. Nchi yetu inasifika kwa kutokuwa na ubaguzi.
 
“Inasifika kwa umoja na sina shaka umoja huu utadumu, nchi yetu inasifika kwa watanzania wote kuwa ndugu.Ni hivi karibuni tu tumeanza kuwa na neno mheshimiwa wakati sote ni ndugu.Nadhani turudi kwenye utaratibu wa ndugu, kila mtu ndugu.
 
“Sasa hivi tunaanza kujenga matabaka kwakutumia neno waheshimiwa.Kuna waheshimiwa na wanaoheshimu lakini hakuna anayeheshimiwa na asiyeshimu.Utakubalika kwa heshima yako , kauli zako na vitendo vyako.”
 
Akiwasilisha mada katika kongamano hilo, Ofisa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu, Victor Rubalagamu alisema ni jukumu la jamii kulinda maadili.
 
Alisema maendeleo ya utndawazi na teknolojia yasiwe sababu ya mmomonyoko wa maadili Bali kiwe chanzo cha kujenga jamii Bora ya Sasa na baadae.
 
Kwa upande wake Sabrina Majikata, muwezeshaji wa malezi ngazi ya taifa, alisema kuwa ujenzi wa maadili na malezi bora ni jukumu la wazazi na walezi.
 
Alieleza kuwa moja ya changamoto za kwa watoto ni harakati za kiuchumi ambazo husababisha wazazi na kukimbizana kutafuta fedha na kusahau jukumu la malezi.
 
‘Tumeacha watoto wanalelewa na wadada wasaidizi ambao nao baadhi yao wamepitia ukatili jambo ambalo wakati mwingine husababisha kulipiza kisasi kwa watoto wanaowalea,” alisema.
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Mapinduzi (CCM) Abdulrahman akisalimiana na viongozi mbalimbali alipowasilka Katika Uwanja wa Ndege wa Katavi kwa ufunguzi wa kongamano la malezi na maadili lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania, mjini Mpanda, Mkoa wa Katavi.
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Mapinduzi (CCM) Abdulrahman akisalimiana na wanachama na wananchi walioshiriki kongamano la malezi na maadili lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania, mjini Mpanda, Mkoa wa Katavi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Taifa Ndg. Ally Hapi akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la malezi na maadili lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania, mjini Mpanda, Mkoa wa Katavi.
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Mapinduzi (CCM) Abdulrahman akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la malezi na maadili lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania, mjini Mpanda, Mkoa wa Katavi. (Picha na Fahad Siraj-CCM)
WANANCHI wakifuatilia kongamano la malezi na maadili lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania, mjini Mpanda, Mkoa wa Katavi.
WASHIRIKI wa kongamano la malezi na maadili lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania, wakiwa wmenuoosha mikono kuunga mkono moja ya jambo lililozungumwa, mjini Mpanda, Mkoa wa Katavi,

About the author

mzalendo