Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Tabora na Katavi kuwa na ushirikiano kati yao, Serikali, Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo Julai 9 na 10,2024 Mkoani Tabora.
Mafunzo kama hayo yamefunguliwa pia Mkoani Katavi na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari na yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 hadi 26, 2024.
“Matokeo bora ya zoezi hili yanategemea uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, Serikali, Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele.
Jaji Mwembegele amewasihi watendaji hao kuwa na ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao na ikiwa wanahitaji ufafanuzi au maelekezo yeyote, wasisite kuwasiliana na Tume.
Aidha, Jaji Mwambegele amesema wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa Vyama vya Siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura jambo ambalo litasaidia kuleta uwazi katika zoezi hilo.
“Mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima. Mawakala hao hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni,”alisema Jaji Mwambegele.
Katika hatua nyingine amesema Tume imetoa vibali kwa Asasi za kiraia 157 kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura na waangalizi wa zoezi la uboreshaji 33 watakao tazama zoezi la uboreshaji.
Jaji Mwambegele amesema Tume inasisitiza kwa Maafisa Waandikishaji kuwa, wanapofika katika maeneo yao, wapewe ushirikiano kwa kuwa ni wadau muhimu.
Mafunzo hayo yanahusisha namna ya ujazaji wa fomu pamoja na kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura (Voters Registration System – VRS) ili waweze kupata uelewa wa pamoja utakaowapa fursa ya kutumia kwa ufasaha mfumo huo pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha wapiga kura.
“Mafunzo haya, yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kisha nao watatoa mafunzo hayo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi ambao ndio watahusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni,” alisema Jaji Mwambegele.
Aidha, Maafisa TEHAMA watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi (Troubleshooting) endapo zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
Mapema kabla ya kuanza mafunzo hayo, washiriki walikua kiapo cha kujitoa uanachama na kile cha kutunza siri.
Tume imetangaza uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika Julai 20, 2024 mkoani Kigoma ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na kauli mbiu ya uboreshaji ni “Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura ni Msingi Wa Uchaguzi Bora”.