Featured Kitaifa

MBETO:CCM IPO TAYARI KUMPOKEA NASSOR MAZRUI.

Written by mzalendo

Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar  Khamis Mbeto Khamis akizungumza katika kikao cha kiutendaji siku za hivi karibuni kisiwani Zanzibar.

NA  MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, amesema kuwa Chama hicho kipo tayari kumpokea Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Nassor Ahmed Mazrui endapo atafukuzwa uanachama katika chama chake.
Kauli hiyo ameitoa leo baada ya kuwepo kwa tetesi za maandalizi ya kufukuzwa kwa kiongozi huyo kwa madai ya kutoridhishwa na kauli yake aliyotoa hivi karibuni ya kumpongeza Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi kwa kazi kubwa ya kuimarisha sekta ya Afya Zanzibar wakati wa uzinduzi wa nyumba za Wafanyakazi wa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoa wa Kusini Pemba.
Katibu huyo alisema amepokea taarifa kutoka katika chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya ACT-Wazalendo, kuwa jana baadhi ya viongozi wa Kamati Kuu ya Chama hicho wamekaa kikao cha siri kujadili kwa kina tuhuma zinazomkabili Naibu Katibu Mkuu huyo Nassor Mzrui na idadi kubwa ya wajumbe hao walipendekeza afukuzwe kwani kauli zake zinaipigia kampeni CCM na kuwatosa kisiasa ACT-Wazalendo.
Mbeto, alisema Chama Cha Mapinduzi ni mwalimu na kinara wa demokrasia nchini hivyo kipo tayari muda wowote kuwapokea viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani wanaokiri kwa vitendo na kuunga mkono kazi nuzi ya kuwaletea maendeleo wananchi bila ubaguzi wa kisiasa.
Katika maelezo yake Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi Mbeto, alisema kitendo cha kiongozi huyo Nassor Mazrui kutamka hadharani kuwa kura ni siri hivyo wananchi wana uhuru wa kuchagua chama kinacholeta maendeleo mbele ya Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi imekuwa ni pigo na majanga kwa ACT-Wazalendo kutokana na sera zao za kubeza,kupotosha na kukosoa  na kutengeneza propaganda chafu ndidi ya CCM na Serikali zake.
“CCM ni kimbilio la wanasiasa na wananchi wote  jambo la msingi ni kuheshimu na kufuata itikadi na sera zetu kwa kutanguliza mbele dhana ya ukweli na uzalendo uliotukuka.
Niwambie wananchi kuwa muda wowote tupo tayari kumpokea kwa mikono miwili Waziri wa Afya na Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Nassor Mazrui, atakapofukuzwa rasmi na Chama chake kwani sababu ya kufukuzwa kwetu tunamuona ni shujaa wa kisiasa na mwenye misimamo isiyoyumba’,alisema Mbeto.
Alieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kila mwananchi yupo huru kutoa maoni hivyo hata ndani ya vyama vya siasa kila kiongozi ana haki ya kutoa maoni yake binafsi na bila kuathiri misimamo ya Chama chake.
Alitoa wito kwa viongozi wengine ndani ya ACT-Wazalendo waendelee kujitokeza hadharani kuunga mkono msimamo wa Nassor Mazrui, kwani hiyo ndio njia pekee ya kujitoa katika jela na utumwa wa kidemokrasia ndani ya chama hicho.
Alisema wakati umefika wa vyama vya upinzani nchini kuachana na siasa za ulaghai na propaganda chafu za upotoshaji badala yake wabadilike na kujenga utamaduni wa kukosoa kwa heshima na kutoa maoni ya kutatua changamoto za wananchi.
Pamoja na hayo Mbeto, alifafanua mapinduzi ya kisiasa ndani ya vyama vya upinzani yataletwa na viongozi wachache wenye dhamira na misimamo imara na kujitolea katika kulinda maslahi ya wananchi wengi  badala ya kundi la viongozi wachache wanaofanya uwakala na udalali wa kisiasa kwa maslahi ya baadhi ya nchi za kigeni.
Sambamba na hayo alisema CCM itaendelea kuheshimu misingi ya kidemokrasia pamoja na kusimamia kwa vitendo sera zake ziendelee kuwa na manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

About the author

mzalendo