Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewaasa watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kufuatilia na kusimamia vema utekelezaji wa Programu mbalimbali za mazingira zilizoandaliwa ili kufikia azma ya kuhifadhi na kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais katika kikao kazi kilichofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage Mkoani Dodoma. Amesema ni vema kuongeza jitihada katika kulinda mazingira kutokana na maeneo mengi nchini kuendelea kukabiliwa na changamoto za uharibifu pamoja na uchafuzi wa mazingira.
Aidha Makamu wa Rais amewasihi watumishi wa Ofisi hiyo kufanya kazi kwa ubunifu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na wananchi katika kufikia azma ya matumizi ya nishati safi ya kupikia. Amewasihi kushirikiana vema na wadau katika kuhakikisha nishati mbadala inapatikana kwa gharama nafuu ili wananchi waweze kumudu matumizi ya nishati hiyo.
Vilevile amewasihi kuwa wabunifu na kuandaa miradi itakayovutia uwekezaji fedha zitazosaidia katika kuhifadhi mazingira nchini. Pia ametoa wito wa kuimarishwa kwa Kituo cha ufuatiliaji wa biashara ya Kaboni ili Taifa liweze kunufaika vema na biashara hiyo inayokua kwa kasi duniani.
Makamu wa Rais amewahimiza watumishi wa Ofisi hiyo kufanya jitihada za kuelimisha wananchi juu ya faida za Muungano na kukabiliana na upotoshaji kuhusu Muuungano hususani katika mitandao ya kijamii. Amewataka kutumia njia za kisasa katika kutoa elimu ikiwemo kutumia Sanaa, Vyombo vya Habari pamoja na kuwahimiza vijana kusoma nyaraka na vitabu mbalimbali vya historia ya Muungano.
Makamu wa Rais ameitaka Idara inayoshughulikia Muungano kushiriki kwa dhati katika vikao vyote muhimu pamoja na kushirikiana vema katika kushughulikia hoja za Muungano zilizobaki.
Makamu wa Rais amewataka watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kulisaidia Taifa kupata maendeleo.